Russia yapinga pendekezo la marufuku ya kupaa ndege Syria
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesema, inapinga pendekezo la kuTENGWA eneo lisiloruhusiwa kupaa ndege ndani ya Syria na kutaka waratibu wa pendekezo hilo kuishirikisha serikali ya Damascus kabla ya kuchukuliwa uamuzi wowote.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Gennady Gatilov amesema, matamshi ya maafisa wa Uturuki na Ujerumani kuhusiana na kutenga eneo lililo marufuku kupaa ndege ndani ya ardhi ya Syria ni uingiliaji wa moja kwa moja wa masuala ya ndani ya nchi hiyo.
Gatilov amesema, hatua kama hiyo inaweza tu kuchukuliwa endapo serikali ya Syria itaridhia na vilevile sharti Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liidhinishe.
Uturuki imetaka kutengwe eneo lililo marufuku ya kupaa ndege karibu na mpaka wake na Syria. Jambo hilo pia linaonekana kuungwa mkono na Ujerumani.