Matokeo ya ukandamizaji nchini Bahrain
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i14770-matokeo_ya_ukandamizaji_nchini_bahrain
Jumuiya mbalimbali za kutetea haki za binadamu zimeendelea kuukosoa utawala wa Aal Khalifa wa nchini Bahrain na wigo wa ukosoaji huo unazidi kuchukua mkondo mpana siku baada ya siku.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 07, 2016 04:13 UTC
  • Matokeo ya ukandamizaji nchini Bahrain

Jumuiya mbalimbali za kutetea haki za binadamu zimeendelea kuukosoa utawala wa Aal Khalifa wa nchini Bahrain na wigo wa ukosoaji huo unazidi kuchukua mkondo mpana siku baada ya siku.

Ukosoajia huo sasa unatolewa hata na asasi za haki za binadamu katika ulimwengu wa magharibi ambazo kwa mrefu zilikuwa zimeunyamazia kimya ukandamizaji unaofanywa na vyombo vya usalama vya Bahrain dhidi ya raia. Joe Stork Naibu Mkurugenzi wa Human Rights Watch Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika amesisitiza kuwa, kuendelea kushikiliwa Nabil Rajab mwanaharakati wa Bahrain kutokana na kutoa maoni katika mitandao ya kijamii ni kukanyaga haki za binadamu kunakofanywa na utrawala wa Manama. 

Kwa upande wake mratibu wa masuala ya Bahrain katika Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International amesema kuwa, kupokonywa uraia Sheikh Issa Qassim mwanazuoni mtajika wa nchi hiyo ni hatua ya kidhulma. Katika miaka ya hivi karibuni vyombo vya mahakama vya Bahrain vimewapokonya uraia makumi ya wanaharakati wa kisiasa wa nchi hiyo vikiwawatuhumu kwa mambo mbalimbali. Shakhsia mashuhuri miongoni mwa waliopokonywa uraia ni Sheikh Issa Qassim mmoja wa Marajii wa Kishia na miongoni mwa viongozi wa harakati ya wananchi wa Bahrain.

Maandamano ya wananchi wa Bahrain

Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, hatua za hivi karibuni za utawala wa Bahrain za kuwapokonya uraia baadhi ya wanaharakati wa nchi hiyo inalenga kuvuruga muundo wa kijamii wa nchi hiyo katika njia ya kuimarisha utawala wake. Kimsingi ni kuwa, utawala wa Aal Khalifa unatumia njama mbalimbali za kuwafukuza nchini humo wanaharakati wa kisiasa na maulama wa nchi hiyo ukijidanganya kwamba, kwa njia hiyo unaweza kudhibiti hali ya mambo na wakati huo huo, kuzima sauti ya wananchi ya kupigania mageuzi.

Kwa mujibu wa marekebisho ya Katiba ya mwaka 2014 nchini Bahrain, utawala wa nchi hiyo una haki ya kumpokonya raia yeyote wa nchi hiyo utakapoona harakati zake zinatishia maslahi ya utawala wa kifalme. kwa hakika hatua hizo zinaonesha kwamba, utawala huo haufikirii kitu kingine bighairi ya kuhakikisha unaendelea kubakia madarakani na sheria za utawala huo zinakinzana dhahir shahir na sheria za kimataifa.

Ayatullah Issa Qassim, mwanazuoni wa Bahrain aliyepokonywa uraia

Jumuiya na asasi za kisheria za kimataifa zimekemea mara chungu nzima hatua hizo za utawala wa Bahrain dhidi ya wanaharakati wa haki za binadamu na hatua yake ya kukataa kushirikiana na jumuiya za kimataifa hususan Umoja wa Mataifa. Fauka ya hayo, asasi hizo zinawataka viongozi wa utawala wa Aal Khalifa waheshimu misingi ya uhuru na kudhamini uhuru wa kusafiri na kuwaachilia huru bila ya masharti yoyote wanaharakati na vilevile kutoa hakikisho la kulinda usalama na uhai wao.

Kuendelea hatua za utawala wa Aal Khalifa za kuhalilisha ukandamizaji wake dhidi ya raia na kuzidi kukiuka kila leo haki za raia kumepelekea kushadidi malalamiko ya wananchi wa nchi hiyo katika miaka ya hivi karibuni. 

Bahrain imekuwa ikishuhudia maandamano ya amani ya wananchi dhidi ya utawala wa Aal Khalifa tangu mwezi Februari mwaka 2011. Wananchi wa Bahrain wanataka marekebisho ya kisiasa, uhuru, uadilifu, kukomeshwa vitendo vya ubaguzi na kuingia madarakani serikali iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia. Utawala wa Bahrain umewanyima wananchi wa nchi hiyo haki zao zote. Aidha ukosoaji wa aina yoyote ile dhidi ya utawala wa Bahrain ni marufuku. Ni kwa msingi huo ndio maana tunashuhudia wanaharakati wengi wa nchi hiyo wakitiwa mbaroni na kuwekwa jela kutokana tu na kupaza sauti ya kutaka mabadiliko ya kisiasa, kisheria na kiuchumi.