Rais Rouhani: Mazungumzo yatumike kutatua migogoro Mashariki ya Kati
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema mazungumzo ya kisiasa yanaonyesha ufahamu ndio njia pekee za kutatua matatizo ya hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati hasa katika Ghuba ya Uajemi.
Rais Rouhani aliyasema hayo Jumatatu wakati alipofanya mazungumzo ya simu na mfalme wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani ambapo alimpa salamu za kheri na fanaka kwa munasaba wa Siku Kuu ya Idul Adha. Rais Rouhani amebaini kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itafanya kila iwezalo kwa ajli ya kufanyika mazungumzo na hivyo amewataka wahusika wote katika eneo pia kujitahidi kwa ajili ya mazungumzo kama hayo.
Rais wa Iran amebainisha masikitiko yake kutokana na kuenea misimamo mikali, vita na ugaidi katika eneo na kuongeza kuwa, 'eneo hili haliko katika hali nzuri'. Aidha amesema ni jukumu la viongozi wa eneo kuwaokoa Waislamu kutokana na tishio la ugaidi na kujitahidi kurejesha uthabiti na kuimarisha udugu miongoni mwa Waislamu.
Emir wa Qatar, kwa upande wake, baada ya kumpa Rais Rouhani salamu za Idi amesema nchi yake ina azma ya kuimarisha uhusiano na Iran katika nyanja zote.
Aidha amesema nchi mbili zinaweza kutumia uhusiano wao kutatua matatizo magumu katika eneo na kuongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nafasi muhimu katika matukio ya eneo.