Askari wa Bahrain washambulia wafuasi wa Sheikh Qassim
Wanajeshi wa utawala wa kifalme Bahrain wametumia gesi ya kutoa machaozi kuwatawanya wafuasi wa Sheikh Issa Qassim waliokuwa wakiandamana wakitaka arejeshewe uraia wake.
Katika maandamano hayo ya Jumamosi, waandamanaji walikusanyika katika kijiji cha Diraz, magharibi mwa mji mkuu Manama, huku wakitoa nara za kumuunga mkono mwanazuoni huyo wa Kiislamu mwenye umri wa miaka 79 ambaye pia ni kiongozi wa kiroho cha chama cha upinzani kilichopigwa marufuku cha Al Wefaq.
Kwa muda wa karibu miezi mitatu sasa wananchi wa Bahrain wamekuwa wakikusanyika kandokando ya nyumba ya Sheikh Issa Qassim katika eneo la Al-Daraz kupinga hatua ya utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal Khalifa kuendeleza mzingiro na kuwatia nguvuni shakhsia na maulamaa wa kidini.
Bahrain imekuwa ikishuhudia maandamano ya amani ya wananchi dhidi ya utawala wa Aal Khalifa tangu mwezi Februari mwaka 2011. Wananchi wa Bahrain wanataka marekebisho ya kisiasa, uhuru, uadilifu, kukomeshwa vitendo vya ubaguzi na kuingia madarakani serikali iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia. Utawala wa Bahrain umewanyima wananchi wa nchi hiyo haki zao zote.