Jeshi la Iran lazionya meli za Saudia zisikaribie maji yake
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran IRGC limetoa onyo kali kwa manowari za Saudi Arabia zinazofanya mazoezi ya kijeshi katika Ghuba ya Uajemi, Ghuba ya Oman na Lango Bahari la Hormuz, dhidi ya kukaribia maji ya nchi hii.
Taarifa ya IRGC imesema kuwa, hatua yoyote ya kichokozi itakayofanywa na meli hizo za kijeshi za Saudia itapokea jibu kali.
IRGC imesema inafuatilia kwa karibu luteka ya Saudia na kusisitiza kuwa mazoezi hayo ya kijeshi yanafanyika kwa shabaha ya kuzusha taharuki na kuhatarisha usalama katika Ghuba ya Uajemi.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran limetilia shaka wakati wa kufanyika luteka hiyo na kuongeza kuwa liko tayari kukabiliana na chokochoko zozote zitakazoanzishwa na jeshi la majini la Saudia dhidi ya taifa hili na kwamba katu Jamhuri ya Kiislamu haitoruhusu maadui kukaribia maji yake.
Abdullah al-Sultan, Kamanda wa Jeshi la Majini la Saudia hata hivyo amesema kuwa maneva hayo ya kijeshi yanafanyika kwa shabaha ya kuongeza ujuzi na maarifa ya kujibu mapigo.
Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Hussein Dehqan mwezi Agosti mwaka huu alionya kuwa, manowari yoyote ya kigeni ikiingia katika maji ya Iran itahesabiwa kama kitendo cha uvamizi ambacho kitapokea jibu kali.