Hamu ya Hamas ya kuimarisha uhusiano na Iran
(last modified Thu, 06 Oct 2016 07:45:48 GMT )
Oct 06, 2016 07:45 UTC
  • Hamu ya Hamas ya kuimarisha uhusiano na Iran

Mmoja wa viongozi wa harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas amesema kuwa harakati hiyo ina hamu ya kuimarisha uhusiano kati yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ismail Ridhwan mwanachama wa ngazi ya juu wa  Hamas amesema kuwa harakati hiyo ina hamu ya kuimarisha uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo siku zote imekuwa ikiunga mkono muqawama na wananchi wa Palestina. Ridhwan amepongeza uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa muqawama huko Lebanon na kusema kuwa, Hamas inaiomba Iran iendeleze uungaji mkono wake huo.

Dr Ismail Ridhwan Mwanachama wa ngazi ya juu wa Hamas

Kuhusu Israel, mwanachama huyo wa ngazi ya juu wa Hamas amesema, utawala huo haujaweza hata kutoa pigo kwa muqawama wa Palestina katika vita vya mfululizo huko Ghaza.

Ismail Ridhwan ameongeza kusema kuwa, muqawama leo hii unao uwezo wa kuzuia uchokozi mpya wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza.

Katika upande mwingine, Wasif Uraiqat jenerali mstaafu na mtaalamu wa masuala ya kistratejia wa Kipalestina amesisitiza kuwa, kushindwa utawala wa Kizayuni kusambaratisha Intifadha ya Quds kunaonyesha kuwa, utawala huo hauwezi kuvunja irada na azma ya wananchi madhlumu wa Palestina kwa kutumia silaha na kutenda jinai dhidi ya raia hao.

Wapalestina wakiendeleza mapambano dhidi ya Wazayuni kwa kutumia manati

 

Tags