Iran yailaani Saudia kwa kuua raia nchini Yemen
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali hatua ya ndege za kivita za Saudia kushambulia mazishi katika mji mkuu wa Yemen San'aa ambapo raia karibu 160 wameuawa na wengine wasiopungua 500 kujeruhiwa.
Katika taarifa, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qassemi amebainisha masikitiko yake kufuatia jinai hiyo ya kinyama na iliyo dhidi ya binadamu ya Saudia. Aidha amesema Iran inafungamana na familia za waliouawa katika kipindi hiki cha majonzi.
Qassemi amekumbusha kuhusu uvamizi wa zaidi ya mwaka moja na nusu wa Saudia dhidi ya Yemen ambapo idadi kubwa ya watu wasio na hatia wameuawa. Amelaani pia kimya cha jamii ya kimataifa kuhusu ukatili wa Saudia dhidi ya wananchi wa Yemen. Aidha Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa wito wa kuhitimishwa mara moja hujuma ya Saudia nchini Yemen sambamba na kufanyika mazungumzo ya Wayemen wote ili kumaliza mgogoro ulioibuliwa nchini humo.
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amelaani vikali mauaji yaliyotekelezwa jana na Saudia dhidi ya raia wasio na hatia Yemen. Akizungumza katika usiku wa saba wa maombolezo ya Muharram, Nasrallah amesema jinai ya Jumamosi Alasiri ya utawala wa Saudia huko San'aa ni jinai ya kuogofya. Aidha amesema si jambo la kushangaza kuona Saudia ikitekeleza jinai kama hivyo.
Kwingineko vyama vya kisiasa Yemen vimelaani vikali ukatili huo wa Saudia na kutaka jamii ya kimataifa ichukue hatua za kivitendo dhidi ya ukoo wa Aal Saud. Mohammad Al Bakhiti mmoja wa viongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema jinai hiyo ya Saudia itapelekea kuingia duru mpya ya mapambano ya watu wa Yemen dhidi ya Saudia.