Askari 15 wa Saudia waangamizwa ndani ya ardhi yao
Kwa akali wanajeshi 15 wa Saudi Arabia wameuawa ndani ya ardhi yao na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen, katika eneo la milima la Jizan, kusini magharibi mwa Saudia.
Habari zinasema kuwa, mbali na askari 15 kuuawa, wengine 40 walijeruhiwa vibaya katika makabiliano makali yaliyojiri jana Jumatano, baada ya mashambulio ya makombora ya jeshi la Riyadh dhidi ya askari wa Yemen kugonga mwamba.
Habari zaidi zinasema kuwa, vikosi vya Yemen vilitekeleza mashambulizi kadhaa dhidi ya vituo vya kijeshi vya Saudia katika eneo hilo la Jizan na kusambaratisha magari kadhaa ya kijeshi ya utawala wa Riyadh. Aidha vikosi hivyo vinavyoungwa mkono na harakati ya Ansarullah vilikishambulia kwa makombora ya balistiki kituo cha kijeshi cha Malik al-Faisal, kilichoko katika mji wa Khamis Mushait eneo la Asir na kituo kingine kilichoko Najran, kusini magharibi mwa Saudia.
Jumapili iliyopita, vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen vilizishambulia kambi mbili za kijeshi za Saudi Arabia mkoani Jizan na kuuwa wanajeshi 25 wa nchi hiyo, ikiwa ni katika kujibu mauaji ya umati ya raia wa Yemen yaliyofanywa na muungano vamizi wa Saudi Arabia huko Sana'a hivi karibuni.
Ndege za kivita za Saudi Arabia Jumamosi jioni ziliushambulia ukumbi mmoja mjini Sana'a nchini Yemen ambako watu wa matabaka mbalimbali walikuwa wamekusanyika katika mazishi na kuua watu 140 na kujeruhi wengine 525.