Uhusiano wa Saudia na Iraq washuka hadi kiwango cha balozi mdogo
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i17416-uhusiano_wa_saudia_na_iraq_washuka_hadi_kiwango_cha_balozi_mdogo
Baada ya serikali ya Iraq kuishinikiza Saudi Arabia imfukuze balozi wake mjini Baghdad kutokana na kuingilia masuala ya ndani ya Iraq, Riyadh imemrudisha nyumbani balozi wake huyo na kupeleka balozi mdogo kushika nafasi yake mjini Baghdad.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 15, 2016 00:25 UTC
  • Uhusiano wa Saudia na Iraq washuka hadi kiwango cha balozi mdogo

Baada ya serikali ya Iraq kuishinikiza Saudi Arabia imfukuze balozi wake mjini Baghdad kutokana na kuingilia masuala ya ndani ya Iraq, Riyadh imemrudisha nyumbani balozi wake huyo na kupeleka balozi mdogo kushika nafasi yake mjini Baghdad.

Shirika la habari la Fars limeripoti habari hiyo na kusema kuwa, Thamer al Sabhan, balozi wa zamani wa Saudia nchini Iraq amerejeshwa nyumbani na nafasi yake kuchukuliwa na balozi mdogo Abdul Aziz al Shammari. 

Vyombo vya habari vya Saudia vilikuwa vimetangaza kuwa, Abdul Aziz al Shammari angeliteuliwa kuwa balozi kamili wa nchi hiyo huko Iraq. 

Mfalme Salman bin Abdul Aziz wa Saudi Arabia

 

Kabla ya hapo Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq ilikuwa imeiandikia barua Saudi Arabia kutaka balozi wake afukuzwe nchini Iraq kutokana na kutoheshima masuala ya kidiplomasia na kuingilia waziwazi masuala ya ndani ya Iraq. 

Huku hayo yakiripotiwa, duru za Iraq zimetangaza kuwa, raia 9 wa Saudia wanasubiri kunyongwa nchini Iraq. Wasaudia hao ni katika wale waliopatikana na hatia ya kufanya vitendo vya kigaidi ndani ya Iraq.  

Televisheni ya Rusia al Yaum imewanukuu maafisa wa Iraq wakitibitisha habari hiyo na kusema kuwa, raia hao tisa wa Saudi Arabia hivi sasa wako katika jela ya Nasiriyah nchini Iraq wakisubiri kutekelezewa adhabu ya kunyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kuwaua kigaidi raia wa Iraq. 

Waislamu wa Kisuni hasa Wakurdi ni miongoni mwa wahanga wakubwa wa jinai za Daesh nchini Iraq

 

Mwaka huu pia serikali ya Iraq imewahi kutekeleza adhabu ya kifo dhidi ya raia watatu wa Saudi Arabia baada ya kuwapata na hatia ya kutenda vitendo vya kigaidi ndani ya Iraq. Ubalozi wa Saudia ulifanya juhudi kubwa za kuzuia kunyongwa Wasaudia hao na wengineo, lakini imeshindwa. 

Vyombo vya usalama wa Iraq vimekuwa vikiwatia mbaroni raia wengi wa Saudia wanachama wa genge la kigaidi la Daesh (ISIS) wanaofanya jinai na mauaji ya kutisha dhidi ya raia wasio na hatia wa Iraq.