Saudia yakiri kuwa ndiyo iliyofanya mauaji ya umati Sana'a Yemen
Saudi Arabia imekiri kuwa ndiyo iliyofanya mashambulizi katika ukumbi ambao ulikuwa umekusanyika mamia ya watu kwa ajili ya maziko kusini mwa Sana'a, mji mkuu wa Yemen Jumamosi iliyopita.
Taarifa iliyotolewa na timu ya Saudia ya kuchunguza mauaji hayo ya umati imesema kuwa, ndege za Saudi Arabia zilifanya mashambulizi hayo kwa kutegemea taarifa za uongo na zisizo sahihi.
Televisheni ya Press TV imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, ndege za kijeshi za Saudia zilifanya mashambulizi katika ukumbi ambao watu wa matabaka mbalimbali walikuwa wamekusayika kushiriki katika maziko ya baba yake waziri wa mambo ya ndani ya Yemen, Jalal al Rowaishan.
Kabla ya hapo serikali ya Saudia ilikanusha vikali jambo hilo na kudai kuwa ndege zake hazikufanya shambulio lolote kwenye eneo hilo siku hiyo ya Jumamosi.
Hata hivyo baada ya kupita wiki moja, yaani leo Jumamosi, timu ya uchunguzi wa tukio hilo inayojulikana kwa kifupi kwa jina la JIAT imekiri kuwa Saudi Arabia ndiyo iliyofanya mauaji hayo ya kutisha dhidi ya mamia ya wananchi wa Yemen.
Shirika la habari la Saudi Arabia SPA limenukuu taarifa ya timu hiyo ikisisitiza kuwa, hatua kali za kisheria lazima zichukuliwe dhidi ya wale wote waliohusika kwenye mauaji hayo kama ambavyo imetaka familia zote za wahanga wa jinai hiyo ya kinyama zilipwe fidia.
Hayo yalikuwa ni mauaji makubwa zaidi kuwahi kufanywa na Saudi Arabai tangu ilipoanzisha uvamizi wake mwezi Machi 2015 huko Yemen. Meya wa mji wa Sana'a, Abdel Qader Hilal ni miongoni mwa watu waliouawa kwenye shambulio hilo.
Ukatili huo unaendelea kulaaniwa hadi leo hii kote ulimwenguni huku shirika la Human Rights Watch likisema kuwa hiyo ni jinai ya wazi ya kivita.
Wakati huo huo ndege moja ya Oman imeelekea mjini Sana'a leo ili kuchukua majeruhi 115 waliojeruhiwa vibaya kwenye mashambulizi hayo. Ikumbukwe kuwa Oman ndiyo nchi pekee ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi iliyokataa kuburuzwa na Saudi Arabia kwenye uvamizi wa Yemen.