Bunge la Kuwait lavunjwa baada ya serikali kujiuzulu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i17557-bunge_la_kuwait_lavunjwa_baada_ya_serikali_kujiuzulu
Mfalme wa Kuwait amelivunja bunge la nchi hiyo punde baada ya serikali kujizulu.
(last modified 2026-05-10T14:24:40+00:00 )
Oct 16, 2016 10:29 UTC
  • Bunge la Kuwait lavunjwa baada ya serikali kujiuzulu

Mfalme wa Kuwait amelivunja bunge la nchi hiyo punde baada ya serikali kujizulu.

Taarifa zinasema, Amir (mfalme) wa Kuwait, Sheikh Sabah al-Ahmad al-Sabah leo ametoa amri ya kuvunjwa bunge la kitaifa la nchi hiyo ili kuandaa mazingira ya uchaguzi wa kabla ya wakati. Imepangwa kuwa uchaguzi wa bunge utafanyika katika kipindi cha siku 60 zijazo katika nchi hiyo ambayo ni kati ya wazalishaji wakubwa wa mafuta ya petroli duniani.

Mji wa Kuwait

Serikali ya Kuwait  mapema ilitangaza kujiuzulu kufuatia msuguano baina yake na bunge. Mgongano baina ya mihimili hiyo miwili ya dola  nchini Kuwait umetokana na hatua ya serikali kuidhinisha nyongeza ya bei ya mafuta ya petroli jambo ambalo wabunge walipinga vikali.

Kushuka kwa bei ya petroli katika soko la kimataifa kumepelekea Kuwait, ambayo hutegemea pato la mafuta, kukumbwa na matatizo makubwa ya nakisi ya bajeti. Kutokana na hali hiyo serikali imelazimika kuwaondolea wananchi ruzuku ya bidhaa na huduma mbali mbali ikiwemo ya petroli.