Taathira ya udiplomasia hasi wa Saudia kuhusiana na Iraq
Kamati ya mahusiano ya bunge nchini Iraq imeitaka Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya nchi hiyo kupinga kuteuliwa na Saudia, Abdulaziz al-Shammari kuwa balozi mdogo mahala pa Thamer al-Sabhan, balozi wa nchi hiyo aliyetimuliwa na Baghdad hivi karibuni.
Khalid al-Asadi, mjumbe wa kamati ya mahusiano ya kigeni katika bunge la Iraq amesema kuwa, Thamer al-Sabhan, balozi wa zamani wa Saudia nchini Iraq alisababisha matatizo makubwa ya kisiasa na kiusalama wakati akiwa nchini humo. Akiweka wazi kuwa balozi huyo wa zamani wa Saudia alifanya ujeuri na kuingilia masuala ya ndani ya Iraq, amesema kuwa ili kuzuia nchi hiyo kutumbukia katika matatizo na migogoro zaidi, wabunge waliamua kuchukua hatua ya haraka ya kumtimua nchini kwao. Inaelezwa kwamba, wakati Thamer al-Sabhan alipokuwa mshauri wa kijeshi katika ubalozi wa Saudia nchini Lebanon, alijihusisha pia na vitendo vya kuibua fitina huku akiwa na mahusiano na baadhi ya makundi ya kitakfiri na kigaidi yaliyokuwa yakiendesha harakati zake nchini humo.
Kiasi kwamba kufikia mwishoni mwa muda wake wa kuhudumu nchini Lebanon alikuwa ameibua machafuko chini humo. Hali ikiwa hivyo kwa al-Sabhan, naye Abdulaziz al-Shammari aliyeteuliwa na Riyadh kuwa balozi mdogo mpya nchini Iraq, alikuwa mshauri wa masuala ya kijeshi wa Saudia nchini Ujerumani. Kwa ajili hiyo tunaweza kusema kuwa, al-Shammari hana tofauti yoyote na balozi wa zamani wa Saudia ambaye utendajikazi wake unatazamiwa kulisababishia matatizo na migogoro mipya taifa la Iraq. Hii ni kwa kuwa, historia ya wawakilishi wa kidiplomasia wanaopendekezwa na Saudia nchini Iraq na katika nchi nyingine za eneo la Mashariki ya Kati, inathibitisha siasa za chuki za Riyadh dhidi ya mataifa hayo. Hii ni katika hali ambayo wangwi wa malalamiko dhidi ya siasa hasi za kigeni za Saudia kuhusiana na utendajikazi mbovu wa Thamer al-Sabhan, balozi wa zamani wa Saudia nchini Iraq umeshadidisha hasira za walio wengi katika eneo. Aidha njama za muda mrefu za utawala wa Aal-Saud za kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine za eneo, ni jambo lingine ambalo linawatia wasi wasi weledi wa mambo. Kitendo cha Saudia cha kuchelewa kumbadilisha Thamer al-Sabhan licha ya malalamiko yaliyokuwepo Iraq, kilikuwa na lengo la kuwasahaulisha Wairaq kunako suala hilo. Hata hivyo kushadidi malalamiko hayo, kuliifanya Riyadh kumteua mtu mwingine mwenye utaalamu wa mauala ya kijeshi ambaye ataweza kucheza mchezo ule ule wa uingiliaji masuala ya ndani ya nchi hiyo.
Hakuna shaka kwamba, Wairaq watatoa radiamali yao kwa siasa hizo za kichochezi za Saudia, kama ambavyo pia hatua ya kupunguzwa udiplomasia kutoka ubalozi hadi ubalozi mdogo, kunabainisha wazi kwamba kamwe Iraq haiwezi kuwa mahala pa kupenyeza siasa mbovu za Saudia. Hivi sasa raia wa Iraq na viongozi wake wana dhana mbaya na siasa za uingiliaji za Saudia nchini mwao na ni kwa ajili hiyo ndio maana wakawa na hamasa maalumu kuhusu siasa za Aal-Saud. Mwenendo wa mabadiliko katika eneo la Mashariki ya Kati unaonyesha kwamba hivi sasa utawala wa kifalme wa Aal-Saud umegeuka na kuwa utawala unaochukiwa zaidi kimataifa kutokana na uungaji mkono wake kwa makundi ya kigaidi na kitakfiri.
Hii ni katika hali ambayo baadhi ya nchi za Kiarabu ambazo awali zilikuwa waitifaki wakubwa wa Aal-Saud katika eneo, hivi sasa zimeamua kujitenga na utawala huo kutokana na siasa mbovu na udiplomasia wa kinafiki unaofutwa na Riyadh.