Wazayuni waendelea kuua watoto wadogo Palestina
Wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni wa Israel wameendelea kufanya jinai dhidi ya Wapalestina kwa kuwashambulia, kuwaua na kuwateka nyara watoto wadogo wa Kipalestina.
Shirika la habari la Qudsuna limeinukuu kamati ya masuala ya mateka wa Palestina ikisema jana Jumatatu kuwa, tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi hivi sasa, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wameshawateka nyara zaidi ya watoto 1000 wa Kipalestina kwa tuhuma zisizo na msingi.
Shirika hilo limeendelea kusema kuwa, wengi wa watoto hao wanaendelea kushikiliwa kwenye korokoro za kiidara (kororo wanazowekwa watu wasiojulikana mashtaka yao), katika jela za kuongofya za Israel.
Wakati huo huo jana asubuhi, wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni waliivamia miji ya al Khalil, Baytullaham na Nablos, katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuwateka nyara wananchi watano wa Palestina na kuwapeleka kusikojulikana.
Uvamizi na kutekwa nyara Wapalestina ni jambo la kawaida kwa utawala wa Kizayuni, na mara kwa mara wanajeshi katili wa Israel wanatumia visingizio visivyo na maana kuwakamata na kuwatesa Wapalestina bila ya hata kujali umri na jinsia zao.
Kwa mujibu wa harakati ya mateka wa Palestina, hivi sasa kuna Wapalestina elfu saba wanaoshikiliwa katika jela 22 tofauti za kuogofya za Israel huku saba kati ya Wapalestina hao wakiwa wanashikiliwa kwenye jela hizo kwa zaidi ya miaka 30 sasa.
Kati ya mateka hao wa Kipalestina, 67 ni wanawake, 400 ni watoto wadogo na sita ni wabunge waliochaguliwa kidemokrasia na wananchi wa Palestina.