UN: Saudia ilikiuka sheria za kimataifa kwa kushambulia waombolezaji Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i17851-un_saudia_ilikiuka_sheria_za_kimataifa_kwa_kushambulia_waombolezaji_yemen
Wasimamizi wa vikwazo vya kimataifa wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa jeshi la Saudi Arabia lilikiuka sheria kwa kushambulia kikao cha waombolezaji nchini Yemen.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Oct 21, 2016 03:59 UTC
  • UN: Saudia ilikiuka sheria za kimataifa kwa kushambulia waombolezaji Yemen

Wasimamizi wa vikwazo vya kimataifa wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa jeshi la Saudi Arabia lilikiuka sheria kwa kushambulia kikao cha waombolezaji nchini Yemen.

Ripoti iliyotumwa na wasimamizi wa vikwazo wa Umoja wa Mataifa katika Baraza la Usalama la umoja huo imesema kuwa, muungano unaoongozwa na Saudia ulikiuka sheria za kimataifa kwa kushambua na kuua raia waliokuwa wakiomboleza mjini San'aa huko Yemen. Ripoti hiyo inasema Saudi Arabia na washirika wake wamekanyaga sheria na majukumu yao ya kimataifa kuhusu watu wasiojiweza na majeruhi vitani. 

Sheria za kimataifa zinapiga marufuku kushambulia watu wenye uwezo mdogo kwa maana ya watu wasio na ulinzi, majeruhi wa vita na wahudumu wa afya. 

Makazi ya raia yanaendelea kushambuliwa Yemen

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mashambulizi yaliyofanywa tarehe 8 mwezi huu wa Oktoba na ndege za kivita za Saudia Arabia dhidi ya watu waliokuwa katika majlisi ya maombolezo mjini San'aa yaliua watu wasiopungua 140 na kujeruhi mamia ya wengine. 

Hadi sasa mashambulizi ya Saudi Arabia na washirika wake yameua raia zaidi ya elfu 10 wa Yemen na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.