Wayemen walaani Umoja wa Mataifa kwa kupuuza jinai za Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i18136-wayemen_walaani_umoja_wa_mataifa_kwa_kupuuza_jinai_za_saudia
Mamia ya watu wa Yemen wameandamana katika mji mkuu, Sana'a kulaani Umoja wa Mataifa kwa kupuuza jinai za kivita za Saudi Arabia dhidi ya nchi yao.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Oct 25, 2016 12:54 UTC
  • Wayemen walaani Umoja wa Mataifa kwa kupuuza jinai za Saudia

Mamia ya watu wa Yemen wameandamana katika mji mkuu, Sana'a kulaani Umoja wa Mataifa kwa kupuuza jinai za kivita za Saudi Arabia dhidi ya nchi yao.

Idadi kubwa ya watu walikusanyika nje ya hoteli moja Sana'a alimokuwa mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa Yemen Ismail Ould Cheikh Ahmad na kumtuhumu kuwa anapendelea utawala wa Saudia.

Waandamanaji hao wametoa nara wakimtaka aondoke Yemen huku wengine wakisema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linahusika na mauaji ya watu wa Yemen.

Aidha waandamanaji wameutuhumu Umoja wa Mataifa kuwa unashirikiana na Saudi Arabia, Marekani na Israel katika vita dhidi ya Yemen. Katika jinai ya hivi karibuni, mnamo  tarehe 8 mwezi huu wa Oktoba  ndege za kivita za Saudia Arabia ziliwashambulia watu waliokuwa katika majlisi ya maombolezo mjini Sana'a na kuua watu wasiopungua 140 na kujeruhi mamia ya wengine. 

Ismail Ould Cheikh Ahmad

Tangu mwezi Machi 2015 na kwa msaada wa baadhi ya nchi za Kiarabu na Marekani, utawala wa kifalme wa Aal Saud unaotawala nchini Saudi Arabia umeanzisha vita dhidi ya Yemen kwa lengo la kumrejesha madarakani kibaraka wake, rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kutoroka nchi Abdrabbuh Mansour Hadi. Hadi sasa Wayemen zaidi ya 10,000 wameuawa katika hujuma hiyo ya Saudia.