Saudia yapunguza tena mishahara ya wafanyakazi wa serikali na wa binafsi
Kwa mara nyingine tena, serikali ya utawala wa kifalme wa Saudi Arabia ambao unakabiliwa na matatizo ya kifedha imepunguza mishahara ya wafanyakazi wa sekta za serikali na za binafsi za nchi hiyo.
Katika uamuzi mpya iliochukua kutokana na kukabiliwa na nakisi ya bajeti, serikali ya Riyadh imepunguza wastani wa mishahara ya wafanyakazi wa ndani katika taasisi zote.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi zilizotolewa na Wizara ya Uchumi ya Saudia, raia wa kigeni wanaofanya kazi katika taasisi za serikali na za binafsi nao pia watahusishwa katika mpango huo.
Inafaa kuashiria kuwa mshahara wa kila mwezi kwa wafanyakazi wa kigeni umeshuka chini ya kiwango cha dola 300, ambacho ni kiwango kidogo mno katika nchi kama Saudi Arabia kutokana na gharama za juu za maisha.
Kupunguzwa mishahara kumewafanya raia wengi wa nchi hiyo wakabiliwe na changamoto nyingi kwa ajili ya kujikimu kimaisha.
Utendaji mbovu wa watawala wa ukoo wa Aal Saud katika nyanja mbalimbali za uchumi umekabiliwa na lawama na ukosoaji mkubwa kupitia mitandao ya kijamii.
Aidha hatua ya utawala huo kujiingiza kijeshi nchini Yemen na kuyasaidia kifedha makundi ya kigaidi dhidi ya nchi za Syria na Iraq imeisababishia matatizo makubwa ya kiuchumi Saudi Arabia…/