Kuafiki Syria mpango wa usitishaji vita
Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imetoa taarifa rasmi na kueleza kwamba serikali ya Damascus inaukubali na itautekeleza mpango wa usitishaji vita uliotangazwa na Marekani na Russia.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa Jamhuri ya Kiarabu ya Syria inakubali kusimamisha hatua za kijeshi kulingana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya Russia na Marekani, lakini itaendelea kupambana na makundi ya kigaidi ya Daesh (ISIS) na Jabhatun-Nusra pamoja na mengine yenye mfungamano na makundi hayo. Hata Moscow na Washington zimetangaza kuwa usitishaji vita huo hautojumuisha makundi ya kigaidi ya Daesh na Jabhatun-Nusra.
Baada ya mashauariano ya hadharahani na faraghani yaliyofanywa baina ya Russia na Marekani, hatimaye makubaliano ya ustishaji vita nchini Syria yametangazwa rasmi.
Marais Vladimir Putin wa Russia na Barack Obama wa Marekani walifanya mazungumzo na mashauriano kwa njia ya simu; na sambamba na hayo mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo, nao pia wamekutana na kufanya duru kadhaa za mazungumzo ili kufikia mtazamo wa pamoja kuhusiana na usitishaji vita nchini Syria.
Kufuatia makubaliano hayo, usitishaji vita utatekelezwa nchini Syria siku ya Jumamosi ya tarehe 27 Februari; na pande mbili za serikali na wapinzani zimetakiwa kuheshimu usitishaji vita huo ili kufungua njia ya mazungumzo ya kitaifa.
Hata hivyo sambamba na tangazo rasmi la serikali ya Syria la kujiunga na mpango wa usitishaji vita, katika jibu na radiamali ya kwanza kwa mpango huo, ujumbe wa wapinzani wa serikali hiyo umetangaza mwishoni mwa kikao chake kilichofanyika mjini Riyadh, Saudi Arabia kuwa wataukubali mpango wa kusitisha mapigano kwa masharti.
Wapinzani hao wamedai kuwa wataheshimu makubaliano ya usitishaji vita endapo mashambulio ya anga ya Russia yatakomeshwa pamoja na kuondolewa mzingiro iliyowekewa miji kadhaa ya Syria.
Takwa hilo la wapinzani linatatiza utekelezaji wa mpango huo wa usitishaji vita. Wapinzani hao wamefika mbali zaidi kwa kutaka wapatiwe hakikisho kimataifa la utekelezaji usitishaji vita na kudai pia kwamba ilikuwa wajulishwe kinachoendelea katika kuandaa rasimu ya makubaliano hayo ili nao pia watoe maoni yao; na si suala hilo kuafikiwa na pande mbili za Russia na Marekani tu.
Baada ya kusimamishwa mazungumzo ya Geneva 3 hadi tarehe Mosi ya mwezi ujao wa Machi, pande za kimataifa zilizokutana karibuni katika kikao cha Munich nchini Ujerumani zilikubaliana kuhusu kupeleka haraka misaada ya kibinadamu nchini Syria, kusimamishwa mapigano na kutekelezwa usitishaji vita; na pande mbili za Moscow na Washington zikapewa jukumu la kusimamia usitishaji vita huo.
Katika miezi ya karibuni, Russia imeingia moja kwa moja katika vita vya ndani nchini Syria kwa kushirikiana na jeshi la nchi hiyo katika kupambana na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh pamoja na makundi mengine washirika wa kundi hilo.
Kushirikiana Marekani na Russia katika suala la usitishaji vita nchini Syria kumedhihirisha na kuweka wazi ukweli huu, kwamba Washington ilikuwa ndiye kiranja wa kukoleza moto wa vita nchini humo katika kipindi chote cha miaka mitano iliyopita. Kukubali Marekani kutangaza usitishaji vita kuna maana ya kukatwa misaada ya silaha na kijeshi ya Washington na shirika la kijeshi la NATO kwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh na makundi mengine waitifaki wa kundi hilo.
Uturuki, Saudia na Qatar, ambazo ni nchi waitifaki wa Marekani katika eneo na ambazo ziliijingiza kwenye vita vya Syria, nazo pia zitapaswa ziheshimu usitishaji vita huo kwa kufuata msimamo wa Washington.
Tokea hapo mwanzo, Marekani iliongoza vita dhidi ya Syria ili kufikia malengo yake kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na kumwondoa madarakani Rais Bashar al-Assad na kuuweka madarakani utawala kibaraka katika nchi hyo.
Hata hivyo mpango huo ulivurugika kutokana na kusimama imara wananchi, jeshi na waungaji mkono wa taifa la Syria na kuifanya Marekani ilazimike kuangalia upya mkakati wake huo.
Katika vita vya niaba vinavyopiganwa na magaidi wa makundi ya kitakfiri ya Daesh na Jabhatun-Nusra, zaidi ya watu laki mbili na nusu wameuawa na zaidi ya milioni 10 wamebaki bila ya makaazi. Katika mazingira hayo, japokuwa serikali ya Damascus imesisitiza kuwa imeukubali mpango wa usitishaji vita ili kuepusha kumwagwa damu zaidi ya wananchi wa Syria na kurejea amani na uthabiti nchini humo, lakini kutokana na utata uliopo kwenye mpango huo wa usitishaji vita hatuwezi kuwa na matumaini juu ya kufanikiwa kwake.../