Michel Aoun; Rais wa 13 wa Lebanon
Baada ya dhoruba na mivutano mingi ya kisiasa, hatimaye Michel Aoun, muitifaki wa harakati ya muqawama ya Lebanon jana alichaguliwa na bunge la nchi hiyo kuwa rais wa 13 wa taifa hilo la Kiarabu.
Baada ya miaka miwili na nusu, hatimaye bunge la Lebanon, likihudhuriwa na wabunge 127 kati ya wabunge wote 128 baada ya mbunge mmoja kujiuzulu, jana lilitimiza akidi; na katika duru ya pili ya upigaji kura lilimchagua Michel Aoun kuwa rais mpya wa nchi hiyo ili kuhitimisha kipindi kirefu zaidi kwa kiti cha urais kubakia kitupu katika historia ya nchi hiyo.
Tangu tarehe 24 Mei, 2014 ambapo kipindi cha uongozi wa aliyekuwa rais wa Lebanon Michel Suleiman kilifikia tamati bunge la nchi hiyo lilifanya vikao vingi katika anga ya hitilafu na mivutano baina ya mirengo ya kisiasa na nipe nikupe za kimaslahi baina ya madola ajinabi, lakini kwa muda wote huo lilishindwa kutimiza akidi ya kuliwezesha kumchagua rais.
Mnamo mwaka 1952 baada ya kujiuzulu Bishara al-Khuri, mwaka 1988 baada ya kumalizika kipindi cha urais wa Amine Pierre Gemayel na mwaka 2007 kufuatia kukamilika kipindi cha uongozi wa Emil Lahud, kiti cha urais wa Lebanon kilibakia wazi kwa muda; lakini kipindi cha mara hii, kilichoanza baada ya kumalizika muda wa uongozi wa Michel Suleiman, ndicho kirefu zaidi kwa Lebanon kubaki bila ya kuwa na rais tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake mwaka 1943 kutoka kwa mkoloni Ufaransa.
Kurefuka mno ombwe la kisiasa katika uendeshaji nchi kuliifanya Lebanon ikabiliwe na hatari ya kukumbwa na hali ya mchafukoge katika nyuga za kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Kuchaguliwa Michel Aoun kuwa rais mpya wa Lebanon kunadhihirisha kuwa muelekeo wa jamii ya Lebanon ni wa muqawama na wa kuunga mkono makundi itifaki kwa muqawama wa nchi hiyo. Tangu awali, Michel Aoun alikuwa akiungwa mkono na mrengo wa Machi 8, unaounda makundi ya Lebanon yanayopinga ubeberu wa Magharibi; na harakati ya muqawama ya Hizbullah imeunga mkono kugombea kwake urais hadi dakika ya mwisho. Uungaji mkono huo umekuwa na taathira chanya katika kufanikiwa Aoun kukalia kiti cha urais wa Lebanon. Kuchaguliwa Michel Aoun kuwa rais wa Lebanon kunaweza kutafsiriwa kuwa ni jibu kali la 'hapana' la Walebanoni kwa miamala ya kibeberu ya madola ya Magharibi na yale ya Kiarabu yenye fikra mgando hususan Saudi Arabia. Kwa sababu mrengo wa Machi 14 wenye ukuruba na utawala wa Riyadh na madola ya Magharibi ulikuwa ukipinga vikali kuchaguliwa Aoun kuwa rais mpya wa nchi hiyo.
Hotuba aliyotoa Michel Aoun mara baada ya kuchaguliwa kuwa rais mpya wa Lebanon kwamba atapambana vikali na makundi ya kigaidi na kitakfiri nchini humo ambayo yanaungwa mkono na Saudi Arabia na ahadi aliyotoa ya kuyakomboa maeneo yaliyosalia ya Lebanon yanayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel pamoja na kuleta mageuzi ya kiuchumi ya nchi nzima ni ishara ya kuingia Lebanon katika awamu na uga mpya wa ujenzi wa nchi na muqawama. Mabadiliko ya kisiasa yaliyotokea Lebanon yameonyesha kwa mara nyingine kuwa Hizbullah ni kiunganishi cha umoja baina ya makundi ya nchi hiyo; na nafasi hiyo na mapenzi unayopata muqawama wa Kiislamu hatimaye umezewesha kukurubishwa pamoja mitazamo ya mirengo mbalimbali na kuandaliwa mazingira ya kumchagua rais mpya.
Ni kutokana na misimamo ya kimantiki ya Hizbullah ndipo baada ya karibu miaka miwili na nusu ya mashauriano kati ya makundi ya Lebanon, hatimaye wiki iliyopita Saad Hariri, waziri mkuu wa zamani na kiongozi wa harakati ya al-Mustaqbal alitangaza kuunga mkono kuchaguliwa Michel Aoun, chaguo la Hizbullah, kuwa rais mpya wa nchi hiyo.../