Israel yapiga marufuku adhana Ukingo wa Magharibi, Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i18901-israel_yapiga_marufuku_adhana_ukingo_wa_magharibi_palestina
Utawala wa Kizayuni wa Israel umepiga marufuku adhana katika misikiti mitatu magharibi mwa eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, linalokaliwa kwa mabavu na utawala huo khabithi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 06, 2016 04:08 UTC
  • Israel yapiga marufuku adhana Ukingo wa Magharibi, Palestina

Utawala wa Kizayuni wa Israel umepiga marufuku adhana katika misikiti mitatu magharibi mwa eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, linalokaliwa kwa mabavu na utawala huo khabithi.

Utawala huo ghasibu umepiga marufuku wito huo wa kuwaita Waumini wa Kiislamu kwenda kutekeleza ibada ya swala katika mji wa Abu Dis, katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan karibu na Quds Tukufu.

Siku moja kabla ya kuanza kutekelezwa marufuku hiyo hapo jana, walowezi wa Kizayuni walifanya maandamano kaskazini mashariki mwa Quds Tukufu, kushinikiza kupigwa marukufu adhana sambamba na kutaka Waislamu katika eneo hilo wazuiwe kutekeleza ibada zao za kila siku.

Quds Tukufu inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni

Ni vyema kukumbusha kuwa, Mwezi Aprili mwaka huu, Waziri wa Waqfu wa Palestina alisema kuwa, utawala wa Kizayuni unafanya njama za kuuyahudisha msikiti wa Ibrahimi katika mji wa Alkhalil na kuongeza kuwa, mwezi Machi mwaka huu, utawala huo ghasibu ulizuia mara 51 kusomwa adhana msikitini humo.

Waziri wa Waqfu wa Palestina alisema kuwa, kitendo cha Wazayuni cha kuzuia kusomwa adhana katika msikiti huo ni muendelezo wa jinai za Wazayuni hao za kuvunjia heshima matukufu ya Waislamu na kuongeza kuwa, wanajeshi wa Israel waliweka kizuizi katika lango kuu la msikiti huo ili kuwazuia Waislamu wasiingie msikitini humo.

Mara kwa mara utawala wa Kizayuni umekuwa ukidai kuwa eti sauti ya adhana inawakera Mayahudi na ndio maana unapiga marufuku kusomwa adhana misikitini.