Misri na Jordan zafanya luteka ya pamoja mjini Akaba
(last modified Sun, 06 Nov 2016 07:47:07 GMT )
Nov 06, 2016 07:47 UTC
  • Misri na Jordan zafanya luteka ya pamoja mjini Akaba

Misri na Jordan zimeanza kufanya luteka ya pamoja katika mji wa bandari wa Aqaba, kusini magharibi mwa Jordan, katika juhudi za kumarisha ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi mbili hizo.

Mazoezi hayo ya kijeshi ya siku 20 yaliyopewa jina "Aqaba 2016" yalianza hapo jana kwa kuvileta pamoja vikosi vya ardhini, baharini na angani vya nchi mbili hizo. Aidha luteka hiyo imevileta pamoja vikosi maalumu vya majeshi ya nchi mbili hizo za Kiarabu.

Imearifiwa kuwa, maneva hayo ya kijeshi yanafanyika kwa lengo la kuimarisha uwezo na utayarifu wa nchi mbili hizo katika kukabiliana na tishio la usalama katika eneo.

Mazoezi ya kijesi

Magenge ya kigaidi yamekuwa yakilishambulia bomba la kusafirishia gesi kutoka eneo la Sinai nchini Misri kuelekea Jordan.

Mwezi uliopita,  mazoezi mengine ya pamoja ya kijeshi baina ya Misri na Russia yaliyobeba kaulimbiu ya "Walinzi wa Urafiki 2016," yalifanyika katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Wizara ya Ulinzi ya Misri ilisema kuwa, zaidi ya wanajeshi 700 wameshiriki katika luteka hiyo ya kijeshi ya siku 10 iliyoanza tarehe 16 Oktoba katika eneo la jangwani la kaskazini magharibi mwa Cairo, mji mkuu wa Misri, na ndani yake kumetumika mbinu mbalimbali za kijeshi katika nyuga tofauti.

Tags