Jeshi la Iraq laingia kaskazini mwa mji wa Mosul
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i18916-jeshi_la_iraq_laingia_kaskazini_mwa_mji_wa_mosul
Wanajeshi wa Iraq wameingia katika eneo la kwanza kabisa la makazi ya watu kaskazini mwa mji wa Mosul, makao makuu ya mkoa wa Nainawa
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 06, 2016 09:46 UTC
  • Jeshi la Iraq laingia kaskazini mwa mji wa Mosul

Wanajeshi wa Iraq wameingia katika eneo la kwanza kabisa la makazi ya watu kaskazini mwa mji wa Mosul, makao makuu ya mkoa wa Nainawa

Shirika la habari la IRIB limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, wanajeshi wa Iraq, leo asubuhi  wameingia katika eneo la kwanza kabisa la makazi ya watu kaskazini mwa Mosul baada ya kuwashinda nguvu wanamgambo wa genge la kigaidi la Daesh (ISIS).

Wakati huo huo Abdulamir Rashid Yarullah, kamanda wa opereseheni ya Nainawa amesema kuwa, jeshi la nchi hiyo limefanikiwa pia kukomboa kijiji cha al Raziqiyyah kutoka mikononi mwa kundi hilo la kitaifiri.

Wananchi wa kujitolea nao wametangaza habari ya kukombolewa eneo la milimani la al Sahaji lililoko umbali wa kilomita 13 magharibi mwa Mosul na hivyo kujiimarisha katika eneo hilo na eneo la al Udayyah la magharibi mwa Mosul.

Wanajeshi wa Iraq katika operesheni ya ukombozi wa Mosul

 

Kamanda mmoja wa vikosi vya kujitolea vya wananchi amesema kuwa, vikosi hivyo viko umbali wa kilomita 30 kutoka mji wa Tel Afar na kufanikiwa kukata mawasiliano baina ya Mosul na eneo hilo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hadi hivi sasa jeshi la Iraq kwa kushirikiana na vikosi vya kujitolea vya wananchi limefanikiwa kukomboa vijiji na maeneo 180 ya mkoa wa Nainawa tangu ilipoanza operesheni ya ukombozi wa mji wa Mosul kaskazini mwa Iraq tarehe 17 mwezi uliopita wa Oktoba.