Vipaumbele vya Rais mpya wa Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i19015-vipaumbele_vya_rais_mpya_wa_lebanon
Rais Michel Aoun wa Lebanon ametangaza vipaumbele na masuala atakayoyapa umuhimu wa kwanza wakati wa kipindi cha miaka sita ya uongozi katika hotuba yake ya kwanza aliyotoa katika Ikulu ya Ba'abda mjini Beirut.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Nov 08, 2016 00:45 UTC
  • Vipaumbele vya Rais mpya wa Lebanon

Rais Michel Aoun wa Lebanon ametangaza vipaumbele na masuala atakayoyapa umuhimu wa kwanza wakati wa kipindi cha miaka sita ya uongozi katika hotuba yake ya kwanza aliyotoa katika Ikulu ya Ba'abda mjini Beirut.

Tangu mwezi Mei 2014 hadi Oktoba 31 mwaka huu, yaani kwa takribani muda wa miezi 30 Lebanon imebaki bila ya rais. Lakini hatimaye tarehe 31 ya mwezi uliopita, bunge lilimchagua Michel Aoun kuwa rais wa 13 wa nchi hiyo.

Katika muda wa chini ya wiki moja Rais Aoun ametangaza masuala atakayoyapa kipaumbele kutokana na umuhimu yaliyonao, katika kipindi cha miaka sita ya urais wake. Katika miaka ya karibuni na hasa baada ya Najib Miqati kujiuzulu wadhifa wa Uwaziri Mkuu mwezi Machi 2013, Lebanon imeshuhudia hitilafu baina ya makundi ya kisiasa za kufadhilisha maslahi ya kimirengo, kichama na kimatapo badala ya maslahi ya taifa. Jambo hilo lilimfanya Tammam Salam, aliyejaza nafasi ya uwaziri mkuu iliyoachwa wazi na Miqati achukue muda wa miezi 11 hadi kuweza kuunda baraza jipya la mawaziri. Hitilafu hizo hizo ndiyo sababu kuu ya kushindwa kumchagua rais mpya kwa muda wa miezi 30.

Najib Miqati (kushoto) na Tammam Salam (kulia)

Kwa sababu hiyo Michel Aoun amesema, kulinda umoja wa kitaifa kwa kufuata misingi ya sheria ndicho kipaumbele chake cha kwanza na akaeleza kwamba shakhsia wa kisiasa wa Lebanon wana wajibu wa kuheshimu katiba ya nchi. Kwa mtazamo wa Aoun kujenga nchi imara na kutekeleza miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu kutawezekana kwa kulinda umoja wa kitaifa na kutanguliza mbele maslahi ya taifa badala ya maslahi ya vyama na mirengo.

Kupambana na ufisadi ni kipaumbele kingine cha Michel Aoun. Katika miaka ya karibuni ubadhirifu wa fedha, biashara ya binadamu na watumwa wa ngono, utoaji rushwa kwa ajili ya kupata fursa za kiuchumi pamoja na mgogoro wa taka ni matukio muhimu ya ufisadi yaliyojiri nchini Lebanon. Rais mpya wa Lebanon ametangaza kuwa ukiukaji wa katiba pia ni aina mojawapo ya ufisadi na akasisitiza kwamba hatoruhusu katiba ya nchi ikiukwe.

Rais Michel Aoun

Michel Aoun amebainisha pia kuwa, kulinda mamlaka ya kitaifa na kujitawala Lebanon ni kipaumbele muhimu zaidi katika sera za nje. Lebanon ni nchi ambayo kwa sababu ya nafasi yake ya kijiografia na kupakana na Syria na Israel ina umuhimu mkubwa katika eneo la Magharibi mwa Asia. Kuwepo harakati imara kama Hizbullah ndani ya nchi hiyo ni sababu nyingine ya umuhimu wa Lebanon katika eneo hili.

Sababu hizi zimezifanya nchi za eneo hasa Saudi Arabia na madola ya nje ya eneo ikiwemo Marekani na Ufaransa yatumie kila njia kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Saudia, Marekani na Ufaransa, ambazo ni waungaji mkono wakuu wa harakati ya al-Mustaqbal inayoongozwa na Saad Hariri ndio wasababishaji wakuu wa mkwamo wa kisiasa uliotokea nchini Lebanon ikiwemo kushindikana kumchagua rais mpya kwa muda wa miezi 30.

Rais Obama wa Marekani (kushoto) na Mfalme Salman wa Saudia (kulia)

Kwa sababu hiyo, katika hotuba yake ya kwanza aliyotoa katika Ikulu ya Ba'abda mjini Beirut, mbali na Rais Aoun kusisitiza kwamba mamlaka ya kujitawala ya taifa la Lebanon yatalindwa bila kuruhusu uingiliaji wa maajinabi na kuwa na utegemezi kwa mataifa ya kigeni, amesema, hamu ya Lebanon ya kuwa na uhusiano wa kirafiki na nchi za Kiarabu haitokuwa sababu ya kuwa na utegemezi kwa nchi hizo.../