Wabahrain waandamana kutaka kuachiwa huru mwanaharakati
Wananchi wa Bahrain wamefanya maandamano ya kushinikiza kuachiwa huru mwanaharakati mashuhuri ambaye alikamatwa na vyombo vya usalama vya Aal-Khalifa mwezi uliopita.
Maandamano hayo ya jana yalifanyika katika kijiji cha Diraz, yapata kilomita 12 magharibi mwa mji mkuu Manama, kutaka kuachiwa huru mwanaharakati Sayyid Alawi Seyed Hussein, ambaye anazuiliwa na utawala huo wa kifalme kwa wiki tatu sasa bila kufunguliwa mashitaka.
Huku wakiwa wamebeba picha ya mwanaharakati huyo na mabango yenye ujumbe, "Sekritarieti Kuu ya Majonzi ya Bahrain; ni mtenda jinai, kamatakamata na ukandamizaji," waandamanaji hao walisikika wakipiga nara wakilaani utawala wa Aal-Khalifa.
Familia ya Sayyid Alawi Seyed Hussein imesema serikali haijawapa ufafanuzi wala maelezo yoyote tangu imkamate mwanaharakati huyo akiwa ofisini kwake Oktoba 24.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, mwezi Juni mwaka huu, utawala wa Aal-Khalifa ulimfutia uraia Sheikh Isa Qassim, mwanazuoni mashuhuri na mkuu wa kimaanawi wa mapinduzi ya watu wa nchi hiyo suala ambalo lilikabiliwa na radiamali kali kutoka ndani na nje ya nchi hiyo.
Sheikh Ali Salman Katibu Mkuu wa Jumuiya ya al-Wifaaq nchini Bahrain ni shakhsia mwingine ambaye amekuwa akizuiliwa na vyombo vya Aal-Khalifa tangu mwezi Julai mwaka jana kwa tuhuma bandia dhidi yake.