Udiplomasia wa Saudia; kuharibu uhusiano wa Iran kieneo na kimataifa
Duru za kisiasa zenye mfungamano na Wasaudia katika siku za hivi karibuni zimezidisha harakati na lobi za kisiasa dhidi ya Iran. Lengo la harakati hizo ni kuiiweka chini ya mashinikizo Iran kieneo na kimataifa.
Saudi Arabia na eti nchi waitifaki wa Riyadh katika eneo hili zingali zinafanya kila ziwezalo kutoa madai yasiyo na msingi wowote ili kuidhihirisha Iran kuwa ni changamoto kwa usalama wa eneo hili. Harakati hizo hata hivyo zinakwenda sambamba na malengo na maslahi ya madola ajinabi katika eneo la magharibi mwa Asia na pia siasa za Israel hapa Mashariki ya Kati. Hii ni kusema kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na nchi nyingine kadhaa za Kiarabu wiki iliyopita huku zikiongozwa na kushawishiwa na Riyadh zilituma barua kwa Umoja wa Mataifa kuwasilisha madai yasiyo na msingi dhidi ya Iran kwamba eti inaingilia masuala ya nchi za eneo hili. Harakati hiyo ya uchochezi ilijadiliwa pia katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi za Kiislamu (OIC) ambayo Saudia ina ushawishi mkubwa ndani yake. Jana Jumapili Mkuu wa Baraza la Uhusiano wa Kimataifa la Nchi za Eneo la Ghuba ya Uajemi (Cogir) alibainisha kuwa wanataka kuifutia Iran uanachama katika OIC. Tariq al Sheikhan alidai kuwa, Tehran inaingilia masuala ya Yemen na kuzitaka nchi zote za Kiislamu kuitenga Iran katika taasisi zote za Kiislamu. Al Sheikhan aliendelea kutoa madai yasiyo na msingi kwa kusema, uingiliaji wa Iran katika masuala ya nchi za Kiarabu umesababisha mivutano na ukosefu wa amani.
Nao ubalozi wa Saudia mjini Cairo Misri umedai sambamba na kutolewa madai hayo yasiyo na msingi kwamba, eti Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendeleza mbinu za kiuhasama katika eneo hili. Ubalozi wa Saudi Arabia huko Cairo jana ulitoa taarifa katika kukamilisha uchochezi wa Saudia na nchi waitifaki wake katika eneo hili na kudai kuwa machafuko na ukosefu wa amani unaoshuhudiwa hivi sasa huko Yemen unatokana na kuendelea uingiliaji wa Iran katika masuala ya Yemen kwa lengo la kuvuruga usalama na utulivu katika eneo hili; na pia eti kuzusha mizozo ya kimadhehebu na kufelisha jitihada za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo.
Hata hivyo weledi wa mambo wanaamini kuwa, Saudi Arabia inaendesha harakati na njama zake zote hizo ikifuatilia malengo mawili ya kistratejia. La kwanza ni kuwa, Riyadh inafanya kila linalowezekana ili kuhalalisha vita vyake vya kichokozi dhidi ya raia wa Yemen. Saudia inafanya kila inaloweza ili kuitangaza Iran kuwa chanzo cha machafuko na kuongezeka hali ya mivutano na hali ya maafa yaliyosababishwa na mashambulizi yake ya mwaka mmoja na nusu huko Yemen. Amma lengo jingine la Riyadh katika harakati hiyo ya kisiasa ni kuzusha mgawanyiko katika uhusiano wa Iran na nchi nyingine jirani za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi. Saudi Arabia iliziweka siasa hizo katika ajenda yake ya kazi tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kuungwa mkono na utawala wa Saddam katika vita vya kulamizimishwa vya miaka minane vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Aidha Saudia iliasisi taasisi kama Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi katika juhudi za kuionesha Iran kuwa eti ni tishio la pamoja kwa nchi za Kiarabu. Saudia haikuacha pia kuingilia kadhia ya nyuklia ya Iran. Riyadh inaendeleza fikra zake hizo katika suala la nyukllia kwani imeonyesha upinzani wake dhidi ya makubaliano ya JCPOA kadiri ilivyoweza. Si hayo tu bali Saudi Arabia imeendelea kutumia masuala hayo yote kama wenzo wa kufikia shabaha zake za kisiasa katika mambo mbalimbali ukiwemo ushindani wa mafuta kati yake na Iran kwenye Jumuiya ya Opec na hata katika suala la Hija pia na kusababisha maafa makubwa kama yale ya Mina.
Ukweli wa mambo ni kuwa, Saudia imekuwa na mialamala ya kiuhasama dhidi ya Tehran. Siasa zisizo za kimantiki za Saudi zimeliathiri eneo zima la Mashariki ya Kati. Hii ni katika hali ambayo migogoro iliyozikumba nchi za magharibi mwa Asia, kuzushwa vita huko Syria, Yemen, Iraq, kuwepo mgogoro huko Lebanon na Bahrain yote hayo ni kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Uungaji mkono wa Saudia kwa makundi ya kigaidi na ya wakufurishaji umepelekea maeneo mengi ya Mashariki ya Kati kuwa medan za vita. Nchi waitifaki wa Riyadh hata hivyo badala ya kupambana moja kwa moja na ugaidi, zimeikabidhi Saudia mustakbali wa nchi zao na hivyo Riyadh kuzitumia nchi hizo kama wenzo wa kisiasa. Matokeo ya siasa hizo hayakuwa na matunda yoyote ghairi ya kushadidisha matatizo katika eneo hili.