Kubadilika misimamo ya Misri kuhusu migogoro ya Mashariki ya Kati
Rais wa Jamhuri ya Misri ametangaza kuwa, nchi yake inayaunga mkono majeshi ya serikali za Syria na Iraq katika mapambano yao dhidi ya ugaidi.
Abdul Fattah al Sisi amesema kuwa, anaunga mkono juhudi za majeshi ya Syria na Iraq katika mapambano yao dhidi ya ugaidi na ametoa wito wa kukabiliana ipasavyo na janga hilo na kukata kabisa vyanzo vya fedha na silaha vya makundi ya kigaidi.
Kuhusu mgogoro wa Syria, Rais Abdul Fattah al Sisi wa Misri amesema kuwa, msimamo wa Cairo kuhusu mgogoro wa nchi hiyo ni kuunga mkono matakwa ya wananchi, kulinda ardhi yote ya Syria na vilevile jitihada za kupatikana mwakafa wa kisiasa wa kukomesha mapigano nchini humo.
Msimamo huo wa Misri wa kuyaunga mkono majeshi ya nchi za Syria na Iraq umetangazwa wakati nchi kadhaa za Kiarabu hususan Saudi Arabia na Qatar zimekuwa zikiyaunga mkono na kuyafadhili kwa hali na mali makundi ya kigaidi yanayopigana na majeshi ya nchi hizo. Serikali ya Misri pia ilishiriki katika vita vya muungano eti wa Kiarabu unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya watu wa Yemen, lakini kiwango cha ushiriki huo kimekuwa cha chini sana, na wachambuzi wa mambo wanasema, Cairo ilishiriki katika vita hivyo vya kidhalimu kwa ajili ya kuendelea kupata misaada ya kiuchumi kutoka Riyadh.
Kwa sasa kunaripotiwa hitilafu kubwa kati ya Saudi Arabia na Misri kuhusu mgogoro wa Syria. Baada ya Rais Abdul Fattah al Sisi kushika hatamu za uongozi nchini Misri, Cairo ilitangaza kuwa mgogoro wa Syria ni suala la ndani linalowahusu Wasyria wenyewe na kwamba mgogoro huo hauwezi kutatuliwa kwa uingiliaji kati wa nchi za kigeni. Hitilafu za Cairo na Riyadh kuhusu mgogoro wa Syria zimeifanya Cairo iunge mkono pendekezo lililotolewa na Russia kuhusu kadhia hiyo, suala ambalo limewakasirisha sana watawala wa kifalme wa Saudia.
Ukweli wa mambo ni kuwa, japokuwa Misri inaihitajia Saudia kutokana na matatizo yake ya kiuchumi lakini tunapaswa kuelewa kuwa, Cairo haiwezi kutupilia mbali nafasi na historia yake na kukubali kuwa chini ya udhibiti wa Saudi Arabia. Inatupasa kukumbusha pia kwamba, Saudia na Misri zinapingana kwa miaka mingi kuhusu masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na juu ya suala la uongozi wa nchi za Kiarabu na pia suala la satua na ushawishi wa taasisi za kidini za nchi hizo mbili katika ulimwengu wa Kiislamu. Masuala hayo daima yamekuwa yakizusha mivutano na mikwaruzano katika uhusiano wa pande hizo mbili.
Kwa muda sasa Misri imepoteza nafasi yake kama nguvu kubwa katika eneo la kaskazini mwa Afrika na kati ya nchi za Kiarabu kutokana na kuongezeka matatizo ya kiuchumi yanayoisumbua serikali ya Abdul Fattah al Sisi. Matatizo ya kiuchumi ya Misri baada ya Rais Abdul Fattah al Sisi kushika hatamu za uongozi na sera za Saudi Arabia hususan upinzani wa watawala wa kifalme wa Riyadh dhidi ya hakati za Kiislamu hususan kundi la Ikhwanul Muslimin, vilitengeneza mazingira ya kuimarishwa zaidi uhusiano wa pande hizo mbili. Kwa utaratibu huo Misri iliipigia mahesabu maalumu misaada ya kifedha ya Saudia. Hata hivyo kupungua kwa pato linalotokana na mauzo ya mafuta la Saudi Arabia baada ya kushuka bei ya bidhaa hiyo katika masoko ya kimataifa, na gharama kubwa zinazotumiwa na utawala huo wa kifalme katika vita vya Yemen na kuyafadhili makundi ya kigaidi na kiwahabi kama lile la Daesh, vimeifanya serikali ya Riyadh ishindwe kutoa misaada ya maana ya kiuchumi kwa serikali ya Cairo. Mbali na hayo sera za kupenda jaha na makuu za utawala wa kifalme wa Saudi Arabia na kutumia misaada ya kifedha kama wenzo na kuilazimisha Misri itekeleze siasa zake katika eneo la Mashariki ya Kati vinaonekana kuwachukiza maafisa wa serikali ya Cairo.
Kwa vyovyote vile, ushahidi uliopo unaonesha kuwa, mgogoro wa Syria umekatiza fungate ya ndoa baina ya serikali za Misri na Saudi Arabia na kupoozesha kabisa uhusiano wa pande hizo mbili.