Wananchi wa Bahrain waandamana kulalamikia ukandamizaji wa utawala wa Aal Khalifa
Maelfu ya wananchi wa Bahrain wameandamana leo wakilalamikia ukandamizaji dhidi ya raia unaofanywa na utawala wa Aal khalifa.
Wananchi hao Waislamu wametangaza himaya na uungaji mkono wao kwa Ayatullah Issa Qassim mwanazuoni wa Kishia anayeshikiliwa na vyombo vya usalama na ambaye utawala wa Manama umetangaza kumpokonya uraia wa nchi hiyo.
Wananchi hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu wamepaza sauti zao na kupinga vikali hatua ya utawala wa Bahrain ya kupiga marufuku Sala ya Ijumaa katika kitongoji cha Diraz kilichoko katika mji mkuu Manama. Washiriki wa maandamana hayo wameutaka utawala wa kifalme wa Aal Khalifa ukomeshe siasa za kipolisi na ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa Kishia nchini humo.
Aidha waandamanaji hao wametaka kuhitimishwa mara moja vitendo vya utawala wa Aal Khalifa vya kuwatia mbaroni kiholela wanaharakati wa nchi hiyo na kuwahukumu vifungo vya miaka mingi jela kwa sababu tu ya kupigania uhuru wa kisiasa na kutaka kuweko utawala wenye ridhaa ya wananchi.
Ikumbukwe kuwa, Bahrain imekuwa ikishuhudia maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa Aal Khalifa tangu Februari mwaka 2011. Matakwa makuu ya wananchi hao ni kuwepo utawala wa kisheria, kukomeshwa ubaguzi wa kimadhehebu, kufanyika mageuzi ya kisiasa na kuheshimiwa haki za binadamu.
Baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa, maelfu ya wananchi wa Bahrain wanashikiliwa jela na katika korokoro za nchi hiyo huku 150 wakiwa wamehukumiwa vifungo vya maisha jela.