Oman: Harakati ya Kiislamu ya Answarullah nchini Yemen sio ya kigaidi
Serikali ya Oman imetangaza upinzani wake dhidi ya pendekezo la Saudi Arabia la kuiweka Harakati ya Kiislamu na ya wananchi ya Answarullah nchini Yemen katika orodha ya pamoja ya wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kuhusiana na ugaidi.
Katika kikao cha leo cha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa baraza hilo kilichofanyika mjini Riyadh Saudia, Oman imetangaza bayana kupinga mienendo ya wanachama wa baraza hilo katika kuiweka Harakati hiyo ya wananchi wa Yemen ya Answarullah katika orodha ya makundi ya kigaidi.

Hii ni katika hali ambayo Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, wamesisitizia kuendelezwa mashambulizi ya kinyama dhidi ya raia wa Yemen. Hayo yanajiri katika hali ambayo hadi sasa jamii ya kimataifa imeendelea kunyamazia kimya jinai za kutisha zinazofanywa na wavamizi wanaoongozwa na Saudia ambazo zimesababisha maelfu ya raia wasio na hatia wakiwemo mamia ya wanawake na watoto kuuawa.

Mashambulizi ya Saudia na vibaraka wake nchini Yemen yanayotekelezwa kwa malengo ya kutaka kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansur Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu wadhifa wake na kukimbilia Riyadh, yameisababishia hasara kubwa nchi hiyo ya Kiarabu.