Mamia ya Wapalestina watekwa nyara na Wazayuni
-
Wanajeshi dhalimu wa Israel wanawateka nyara hata watoto wadogo wa Kipalestina.
Kituo cha Kufuatilia Masuala ya Mateka wa Palestina kimesema kuwa, mamia ya Wapalestina wametekwa nyara na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika kipindi cha mwezi ulioisha wa Novemba.
Televisheni ya Press TV imekinukuu kituo hicho kikisema jana kuwa, Wapalestina 527 wametekwa nyara na wanajeshi wa utawala dhalimu wa Israel katika mwezi Novemba pekee. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mateka 120 kati ya hao 527 ni watoto wadogo.
Taarifa ya kituo hicho imeongeza kuwa, sehemu kubwa ya Wapalestina hao wametekwa nyara na wanajeshi wa Kizayuni katika eneo la mashariki mwa mji mtakatifu wa Baytul Muqaddas.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hivi sasa kuna karibu Wapalestina elfu saba kwenye jela za kuogofya za utawala wa Kizayuni wa Israel.
Wanajeshi katili wa Kizayuni walilivamia eneo la mashariki mwa Ramallah juzi Ijumaa na kuwateka nyara Wapalestina wanne kwa madai ya kushiriki katika opereseheni dhidi ya Wazayuni.
Kila leo wanajeshi wa Israel wanawashambulia vijana na mabarobaro wa Kipalestina, kuvamia nyumba zao na kuwateka nyara na halafu kuwapeleka maeneo yasiyojulikana na kuwaweka katika mazingira ya mateso na unyanyasaji mkubwa.