Jeshi la Iraq laendelea kukomboa maeneo ya Mosul na kuwafurusha Daesh
Msemaji wa komandi ya oparesheni ya pamoja ya Iraq ametangaza habari ya mpango mpya ulioandaliwa na jeshi la nchi hiyo kwa ajili ya kuliangamiza kundi la kigaidi la Daesh huko Mosul.
Brigedia Jenerali Yahya Rasool ameashiria oparesheni ya jeshi la Iraq ya kuukomboa mji wa Mosul kutoka mikononi mwa magaidi na kueleza kuwa, komandi hiyo itatumia stratejia na mbinu mbalimbali ili kuharakisha mji wa Mosul unakombolewa na magaidi wa Daesh wanatimuliwa. Brigedia Jenerali Rasool ameongeza kuwa, wanajeshi wa Iraq wanazidi kupata ushindi na mafanikio katika kukabiliana na Daesh.
Wakati huo huo Abdul Amir Rashid Yarallah, kamanda wa oparesheni ya Nainawa amesema kuwa vikosi vya jeshi la Iraq vimewafurusha magaidi katika maeneo 23 huko Mosul. Yarallah ameongeza kuwa, eneo la al Kifayat Thalitha huko Mosul pia limekombolewa kutoka kwa wapiganaji wa kundi la Daesh na sasa bendera za Iraq zinapepea juu ya nyumba za eneo hilo.
Oparesheni ya kuukomboa mji wa Mosul kutoka kwa magaidi wa kundi la Daesh ilianza Oktoba 17 mwaka huu kwa amri ya Waziri Mkuu wa Iraq Haidar al Abadi.
Vikosi vya usalama vya Iraq ambavyo vinajumuisha jeshi, polisi, makundi ya kujitolea ya wananchi na wapiganaji wa Kikurdi wa Pishmerga hadi kufikia sasa vimeweza kuyakomboa makumi ya maeneo na vijiji huko Mosul kutoka kwa Daesh tangu kuanza oparesheni ya kuukomboa mji huo.