Ulinzi waimarishwa katika mpaka wa Iraq na Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i21067-ulinzi_waimarishwa_katika_mpaka_wa_iraq_na_syria
Duru za usalama nchini Iraq zimetangaza kuwa, usalama umeimarishwa katika mpaka wa nchi hiyo na Syria.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Dec 09, 2016 04:09 UTC
  • Ulinzi waimarishwa katika mpaka wa Iraq na Syria

Duru za usalama nchini Iraq zimetangaza kuwa, usalama umeimarishwa katika mpaka wa nchi hiyo na Syria.

Mtandao wa habari wa al Nashra umemnukuu Jawad al Talibawi, mmoja wa viongozi waandamizi wa vikosi vya kujitolea vya wananchi maarufu kwa jina la al Hashdu al Shaabi akisema hayo jana jioni na kuongeza kuwa, baada ya kukombolewa eneo la Tal Abta kutoka mikononi mwa genge la kigaidi la Daesh, sasa mpaka wa Iraq na Syria umedhibitiwa kikamilifu.

Amesema, kukombolewa eneo hilo kumefungua njia ya kukombolewa maeneo mengine yaliyoko karibu na mpaka wa Iraq na Syria kama vile al Biaj na al Qeyrawan na kumepelekea kudhaminiwa usalama wa eneo lote la mpakani.

Jeshi la Iraq likiendeleza mapambano dhidi ya magaidi wa Daesh

 

Kamanda huyo wa vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Iraq amesema pia kuwa, kundi la kigaidi la Daesh limepata pigo kubwa katika operesheni ya ukombozi wa eneo la Tal Abta na kadiri siku zinavyopita ndivyo magaidi wa Daesh wanavyozidi kuzingirwa na kubanwa kila upande.

Kwa mujibu wa taarifa ya duru za usalama za Iraq, operesheni ya jana Alkhamisi ya vikosi vya nchi hiyo ilifanikiwa kuangamiza makumi ya magaidi wa Daesh na kuteketeza magari kadhaa yaliyokuwa yametegwa mavomu.

Kundi la kigaidi la Daesh linatumia mbinu ya kuripua magari yaliyosheheni mabomu ili kukabiliana na kipigo cha mfululizo inachokipata kwenye medani za vita.