Syria yalaani azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Syria imelaani azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linalotaka kusimamishwa "mara moja" mapambano dhidi ya makundi yanayobeba silaha ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Akizungumza mara baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitisha kwa kura 122 za 'ndiyo' na 13 za 'hapana' azimio la kuitaka serikali ya Damascus isitishe mapambano yake dhidi ya magaidi wa kitakfiri, zifunguliwe njia za kufikisha misaada ya kibinadamu nchini kote na kuhitimishwa mizingiro yote iliyowekwa ukiwemo mzingiro dhidi ya mji wa Aleppo, mwakilishi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar Al-Jaafari amelilaani vikali azimio hilo la Baraza Kuu.
Katika miezi ya karibuni vikosi vya jeshi la Syria vimefanikiwa kuyazingira maeneo ya mashariki mwa mji wa Aleppo; na kutokana na mafanikio yaliyopatikana, maeneo hayo yanakaribia kukombolewa kikamilifu kutoka mikononi mwa makundi ya kitakfiri.
Iran, Russia na China ni miongoni mwa nchi zilizopinga azimio hilo.
Bashar Al-Jaafari amemkosoa mwakilishi wa Canada pamoja na washirika wake kwa kukiuka mamlaka ya kuijtawala ya Syria kwa kuwasilisha ombi la kuitishwa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa bila ya kushauriana na mwakilishi wa Syria na kusisitiza kuwa azimio hilo ni la kisiasa, halina ulazima wa kutekelezwa na linakiuka Hati ya Umoja wa Mataifa.
Mwakilishi wa Syria katika Umoja wa Mataifa amesema, kupitishwa azimio hilo hakutoizuia serikali ya Damascus na waitifaki wake kuendeleza mapambano dhidi ya ugaidi na akaahidi kwamba karibuni hivi mji wote wa Aleppo utadhibitiwa na vikosi vya serikali.
Al- Jafari amefafanua zaidi kwa kusema: "Kwa mara nyingine nazihakikishia nchi zinazounga mkono ugaidi mjini Aleppo kwamba jeshi la Syria hadi sasa limeshakomboa asilimia 93 ya maeneo yaliyokuwa yakidhibitiwa na magaidi; hivyo mchezo wao wa ugaidi wa umwagaji damu nchini Syria na Aleppo umeshafikia tamati"…/