Mufti wa Lebanon ataka ulimwengu uunge mkono kadhia ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i21196-mufti_wa_lebanon_ataka_ulimwengu_uunge_mkono_kadhia_ya_palestina
Mufti mkuu wa Lebanon ametoa wito kwa walimwengu kuunga mkono kadhia ya Palestina.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Dec 11, 2016 04:32 UTC
  • Mufti wa Lebanon ataka ulimwengu uunge mkono kadhia ya Palestina

Mufti mkuu wa Lebanon ametoa wito kwa walimwengu kuunga mkono kadhia ya Palestina.

Sheikh Abdul Latif Derian ameashiria hatua na vitendo vya kibaguzi vya utawala vamizi wa Israel dhidi ya taifa madhulumu la Palestina  na kubainisha kwamba, kadhia ya Palestina ni suala kuu na la msingi katika ulimwengu wa Kiarabu bila kujali Waislamu wala Wakristo.

Mufti wa Lebanon amezitaka nchi zote za Kiarabu na asasi za kimataifa kudumisha umoja na mshikamano wao na kutetea kusimama kidete taifa madhulumu la Palestina kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao umekuwa ukitenda jinai kila uchao dhidi ya wananchi hao wasio na ulinzi.

Mufti wa Lebanon ameeleza kuwa, wapigania uadilifu na watu wenye dhamira safi wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuiunga mkono kadhia ya Palestina na kutetea hatua ya wananchi wa Palestina ya kusimama kidete kuilinda na kuihami ardhi yao mbele ya utawala ghasibu wa Israel.

Wanajeshi wa Israel wakivamia msikiti wa al-Aqswa

Hayo yanajiri katika hali ambayo, katika miezi ya hivi karibuni utawala wa Kizayuni wa Israel umeshadidisha hujuma na njama zake dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Ikumbukwe kuwa, tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka uliopita wa 2015 hadi sasa maeneo mbalimbali ya ardhi za Palestina yamekuwa yakishuhudia wimbi la malalamiko ya upinzani dhidi ya siasa za kichokozi za Israel. Wimbi hilo la malalamiko limekuwa maarufu kwa jina la Intifadha ya Quds. Hadi sasa zaidi ya Wapalestina 200 wameshauawa shahidi tangu ilipoanza Intifadha ya Quds mwezi Oktoba mwaka jana.