Wabahrain waandamana dhidi ya kesi ya Sh. Salman inayosikilizwa leo
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i21268-wabahrain_waandamana_dhidi_ya_kesi_ya_sh._salman_inayosikilizwa_leo
Wananchi wa Bahrain wamefanya maandamano katika barabara za nchi hiyo usiku wa kuamkia leo kuulani utawala wa Aal-Khalifa wa nchi hiyo, ambapo hii leo mahakama ya nchi hiyo inatazamiwa kusikiliza kesi ya Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa Harakati ya Kitaifa ya Kiislamu ya Al-Wifaq, iliyopigwa marufuku na utawala huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 12, 2016 04:20 UTC
  • Wabahrain waandamana dhidi ya kesi ya Sh. Salman inayosikilizwa leo

Wananchi wa Bahrain wamefanya maandamano katika barabara za nchi hiyo usiku wa kuamkia leo kuulani utawala wa Aal-Khalifa wa nchi hiyo, ambapo hii leo mahakama ya nchi hiyo inatazamiwa kusikiliza kesi ya Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa Harakati ya Kitaifa ya Kiislamu ya Al-Wifaq, iliyopigwa marufuku na utawala huo.

Mamia ya wananchi wa Bahrain ambao walikuwa wamebeba mabango na picha za Sheikh Salman, wameshiriki maandamano hayo katika vijiji vya Diraz, al-Markh na Saar sawia na mji wa Bilad al-Qadeem, wakitaka kuachiwa huru kiongozi huyo wa Kiislamu.

Mwezi Juni mwaka huu, Mahakama ya Rufaa ya Bahrain ilizidisha hukumu ya kifungo cha jela cha miaka minne aliyokuwa amekatiwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu ya Kitaifa ya al Wifaq ya Bahrain hadi miaka tisa.

Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa al-Wifaq

Sheikh Salman, Katibu Mkuu wa Al-Wifaq, ambayo ndiyo harakati kuu ya upinzani nchini Bahrain alitiwa nguvuni mwezi Desemba mwaka 2014 baada ya kutoa hotuba kadhaa za kupinga siasa za utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa.

Haya yanajiri siku chache baada ya raia watatu wa nchi hiyo kuhukumiwa adhabu ya kifo na mahakama ya nchi hiyo huku raia wengine 11 wakihukumiwa kifungo cha maisha jela. Aidha ripoti zinasema kuwa, raia wengine wanane wa Bahrain walipokonywa uraia hivi karibuni. 

Maelfu ya wananchi wa Bahrain wanashikiliwa katika magereza na korokoro za nchi hiyo huku 150 kati yao wakiwa wamehukumiwa vifungo vya maisha jela.

Polisi wakiwarushia mabomu ya kutoa machozi waandamani kijijini Diraz

Ikumbukwe kuwa, Bahrain imekuwa ikishuhudia maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa Aal Khalifa tangu Februari mwaka 2011. Matakwa makuu ya wananchi hao ni kuwepo utawala wa kisheria, kukomeshwa ubaguzi wa kimadhehebu, kufanyika mageuzi ya kisiasa na kuheshimiwa haki za binadamu.