Maeneo ya Halab nchini Syria yazidi kupata utulivu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i21688-maeneo_ya_halab_nchini_syria_yazidi_kupata_utulivu
Mji wa Halab wa kaskazini mwa Syria umezidi kuwa na utulivu baada ya makundi ya kigaidi kufurushwa mjini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 19, 2016 00:54 UTC
  • Maeneo ya Halab nchini Syria yazidi kupata utulivu

Mji wa Halab wa kaskazini mwa Syria umezidi kuwa na utulivu baada ya makundi ya kigaidi kufurushwa mjini humo.

Mwandishi wa Radio Tehran ameripoti kuwa, zoezi la kutoka magaidi mashariki mwa mji wa Halab liliendelea jana Jumapili.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mabasi yasiyopungua 25 yametumwa mashariki mwa mji wa Halab kwa lengo la kuwaondoa magaidi waliobakia na kuwapeleka maeneo mengine kulingana na makubaliano maalumu yaliyofikiwa baina ya serikali ya Syria na magaidi hao.

Makubaliano hayo yalifikiwa Alkhamisi iliyopita lakini jeshi Syria lilisimamisha zoezi hilo baada ya makundi ya kigaidi kutoheshimu makubaliano hayo ikiwa ni pamoja na kukataa kuwaruhusu wananchi waliozingirwa na magaidi hao kuelekea upande wa jeshi la serikali.

Baadhi ya wanamgambo waliojisalimisha kwa serikali nchini Syria

 

Duru za habari za Syria zimesema kuwa, zaidi ya magaidi elfu tisa na familia zao wameshaondoka mashariki mwa Syria tangu siku ya Alkhamisi. Jeshi la serikali ya Syria limesema, watu wenye silaha hawatoshambuliwa na wataruhusiwa kutoka maeneo ya mashariki mwa mji wa Halab iwapo tu magaidi wenzao wataacha kuwazingira raia wa vijiji vya Fua na Kafarya vilivyoko kwenye viunga vya Idlib, kaskazini magharibi mwa Syria. Maeneo hayo mawili yazingirwa na mgaidi hao kwa karibu miaka mitatu sasa.

Televisheni ya al Ikbariya ya Syria imetangaza kuwa, magaidi waliyashambulia mabasi matano yaliyoingia kwenye vijiji vya Fua na Kafarya suala ambalo lilikasirisha jeshi la Syria na kusimamisha zoezi la kuwafungulia njia ya kutoka magaidi huko mashariki mwa mji wa Halab.