Lebanon yatangaza baraza jipya la mawaziri linaoongozwa na Hariri
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i21700-lebanon_yatangaza_baraza_jipya_la_mawaziri_linaoongozwa_na_hariri
Lebanon imetangaza baraza jipya la mawaziri linaloongozwa na Waziri Mkuu, Saad al-Hariri, wiki 6 baada ya kuchaguliwa Rais Michel Aoun.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 19, 2016 03:55 UTC
  • Lebanon yatangaza baraza jipya la mawaziri linaoongozwa na Hariri

Lebanon imetangaza baraza jipya la mawaziri linaloongozwa na Waziri Mkuu, Saad al-Hariri, wiki 6 baada ya kuchaguliwa Rais Michel Aoun.

Televisheni ya serikali iliyatangaza hayo jana Jumapili na kuongeza kuwa, baraza hilo litakuwa na mawaziri 30. Baadhi ya walioteuliwa kushika nyadhifa hizo ni Gebran Bassil, Waziri wa Mambo ya Nje, Ali Hassan Khalil, Waziri wa Fedha, Nouhad Machnouk,  Waziri wa Mambo ya Ndani huku Wizara ya Ulinzi ikipewa Yacoub al-Sarraf.

Waziri Mkuu wa Lebanon, Saad Hariri akiongea na waandishi wa habari

Saad al-Hariri, Waziri Mkuu wa Lebanon amesema serikali hiyo imejumuisha watu wa jamii na matabaka yote ya nchi, licha ya chama cha Kikristo cha Phalangist kususia wizara iliyotengewa.

Mapema mwezi uliopita, Rais Michel Aoun wa Lebanon ambaye ni muitifaki wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah, alimteua Hariri, kiongozi wa harakati ya al-Musatqbal kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Katiba ya Lebanon, Rais wa nchi anapasa kutoka miongoni mwa Wakristo wa Maroni, Waziri Mkuu  jamii ya Waislamu wa Kisunni na Spika wa Bunge awe anatoka jamii ya Waislamu wa Kishia.

Michel Aoun, Rais wa Lebanon

Baada ya kupita zaidi ya miaka miwili ya mkwamo wa kisiasa, Oktoba 31, Bunge la Lebanon lilifanya kikao chake cha 46 cha upigaji kura na hatimaye kumchagua Michel Aoun mwenye umri wa miaka 81 kuwa rais mpya wa nchi hiyo.