Magaidi Mosul, Iraq wanaongozwa na maafisa wa kijeshi wa nchi jirani
Ushahidi umebaini kuwa, maafisa wa kijeshi na kijasusi wa nchi za eneo la Mashariki ya Kati wanahusika katika kuwaongoza na kuwaelekeza magaidi katika mji wa Mosul nchini Iraq.
Hayo yamedokezwa na Sayyid Ammar Hakim, Mwenyekiti wa Muungano wa Kitaifa wa Waislamu wa Madhehebu ya Shia nchini Iraq ambaye ameongeza kuwa, maafisa hao wa kijeshi na kijasusi wanawaongoza magaidi mjini Mosul na pia katika miji mingine ya Iraq.
Katika mahojiano yake na Shirika la Utangazaji la Iran, IRIB, Sayyid Hakim amekosoa kuwepo majeshi ya kigeni katika eneo la Mashariki ya Kati na kusema majeshi hayo hayasaidii chochote bali ni chanzo za ukosefu wa usalama.
Serikali ya Iraq imekuwa ikiituhumu Saudi Arabia kuwa inawaunga mkono magaidi nchini humo.
Mwanasiasa huyo wa ngazi za juu nchini Iraq amewakosoa wale wanaopinga suala la kuundwa kikosi cha kujitolea cha wananchi nchini humo maarufu kama al Hashad al Shaabi na kusema kuwa kikosi hicho kimekuwa na nafasi muhimu katika vita dhidi ya magaidi.
Amesema wapiganaji wa al Hashad al Shaabi nchini Iraq wanalinda maslahi ya taifa na hivyo watu wengine hawana haki ya kuhoji kuhusu kikosi hicho.
Sayyid Ammar Haki ameongeza kuwa wananchi kutoka kaumu na madhehebu zote za Iraq wamehusika katika kuunda jeshi la kujitolea la al Hashad al Shaabi. Amesema jeshi hilo la wananchi linajumuisha Waislamu wa madhehebu ya Shia na Suni na kaumu za Waizadi, Wakurdi, Watorkman na Wakristo na kwamba jeshi hilo ni nembo ya kitaifa.