Uingiliaji wa madola ya kigeni, sababu ya kurefuka ukombozi wa Mosul
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i22171-uingiliaji_wa_madola_ya_kigeni_sababu_ya_kurefuka_ukombozi_wa_mosul
Sayyid Ammar al Hakim, Mkuu wa Muungano wa Taifa wa Mashia wa Iraq amesema, ushahidi unaonesha kuwa, kuweko maafisa wengi wa kijeshi na kijasusi wa nchi za eneo la Mashariki ya Kati huko Iraq, kunazorotesha juhudi za nchi hiyo za kupambana na magaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 26, 2016 08:38 UTC
  • Sayyid Ammar al Hakim, Mkuu wa Umoja wa Taifa wa Mashia wa Iraq
    Sayyid Ammar al Hakim, Mkuu wa Umoja wa Taifa wa Mashia wa Iraq

Sayyid Ammar al Hakim, Mkuu wa Muungano wa Taifa wa Mashia wa Iraq amesema, ushahidi unaonesha kuwa, kuweko maafisa wengi wa kijeshi na kijasusi wa nchi za eneo la Mashariki ya Kati huko Iraq, kunazorotesha juhudi za nchi hiyo za kupambana na magaidi.

Ikumbukwe kuwa, operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul, makao makuu ya mkoa wa Nainawa nchini Iraq kutoka mikononi mwa magaidi wa Daesh, ilianza tarehe 17 Oktoba mwaka huu kwa amri ya Waziri Mkuu wa Iraq, Haydar al Abadi. Katika siku za mwanzoni mwa opereseheni ya ukombozi wa Mosul, jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi vilipata ushindi mkubwa na wa haraka kiasi kwamba vijiji na maeneo mengi ya pambizoni mwa Mosul yalikombolewa kwa kasi kubwa na wanajeshi wa Iraq kufanikiwa kuingia mjini Mosul. Baadhi ya wachambuzi wa mambo walitabiri kuwa operesheni ya ukombozi wa Mosul ingelimalizika hata kabla ya mwishoni mwa mwaka huu wa 2016.

Hata hivyo kasi ya ushindi katika opesheni hiyo imepungua na kuna sababu mbalimbali zinatolewa kuhusu jambo hilo. Moja ya sababu kuu ni uingiliaji wa madola ya kigeni na uungaji mkono wao kwa kundi la kigaidi la Daesh licha ya kidhahiri kuonesha kuwa yanapambana na magaidi hao. Viongozi mbalimbali wa Iraq wamesema mara nyingi kuwa, madola ya kigeni yanaingilia kikamilifu masuala ya nchi hiyo ikiwemo kadhia nzima ya ukombozi wa Mosul.

Wanajeshi wa Iraq wakisherehekea ushindi

 

Sayyid Ammar al Hakim, Mkuu wa Umoja wa Taifa wa Mashia wa Iraq amesema, kuna ushahidi madhubuti unaothibitisha kwamba baadhi ya nchi za eneo la Mashariki ya Kati zimetuma maafisa wao wa kijeshi na kijasusi kwenda kuwasaidia magaidi wa Daesh na kusimamia operesheni zao huko Mosul. Kabla ya hapo pia, Haydar al Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq alisema tarehe 4 Disemba kuwa Uturuki imetuma wanajeshi wake katika mkoa wa Nainawa bila ya idhini ya serikali ya Iraq kwa shabaha ya kuyapa mafunzo ya kijeshi makundi yenye silaha.

Swali linalojitokeza hapa ni kwamba, kwa nini nchi za kigeni hususan nchi kama Marekani, Uturuki na Saudi Arabia zinakwamisha operesheni za kukombolewa kikamilifu Mosul kutoka mikononi mwa magaidi wa Daesh? Majibu ya swali hilo yanapatikana kwa kuzingatia hali ilivyo ndani ya Iraq na hali ya eneo la Mashariki ya Kati hivi sasa. Kwa upande wa hali ya ndani ya Iraq, suala la kuwa na nguvu serikali ya nchi hiyo halizifurahishi hata kidogo nchi kama Uturuki na Saudi Arabia. Katika upande mwingine nchi hizo zinaona namna vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Iraq vilivyotoa mchango mkubwa katika vita dhidi ya ugaidi. Hadi hivi sasa vikosi hivyo vya kujitolea vimeonesha uwezo mkubwa wa kuwafurusha magaidi katika ardhi yote ya Iraq. Hata hivyo madola ya kigeni kama vile Saudi Arabia yanaeneza propaganda kuwa vikosi hivyo vinawakandamiza Masuni wa Iraq, madai yasiyo na mashiko ambayo yamekanushwa haraka mno na viongozi wa Iraq na shakhsia wengine mbalimbali wa nchi hiyo.

Maafisa wa Iraq wakikagua kaburi la umati la watu waliouliwa kinyama na magaidi wa Daesh

 

Sayyid Ammar al Hakim, Mkuu wa Umoja wa Taifa wa Mashia wa Iraq amesema, vikosi vya kujitolea vya wananchi vinafanya opereseheni zake kwa baraka kamili za Bunge na Serikali ya nchi hiyo na ni sehemu ya vikosi vya ulinzi vya Iraq. Ni vikosi vilivyoundwa na wananchi wenyewe wa Iraq, hivyo dola lolote la kigeni halina haki ya kuingilia maamuzi ya wananchi wa Iraq. Pia amesema, kinyume kabisa na propaganda za maadui wa taifa la Iraq, vikosi vya kujitolea vya nchi hiyo ni vya wananchi wote, havihusiana na kundi na madhehebu fulani tu ya wananchi. 

Tukija katika upande wa kieneo pia tutaona kuwa, ushindi wa jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Syria na waitifaki wao katika operesheni ya Halab na kufanikiwa kuwafurusha magaidi waliokuwa wanasaidiwa na madola ya kigeni kama Marekani, Israel, Saudi Arabia, Uturuki, Qatar n.k, limekuwa ni pigo kubwa kwa wapinzani wa serikali ya Rais Bashar al Assad wa Syria. Hivyo nchi hizo sasa hivi zinafanya kila liwezekanalo kuzuia kukombolewa kikamilifu mji wa Mosul nchini Iraq ambayo ni jirani na Syria.