Makubaliano ya kutekeleza usitishaji vita kote nchini Syria yafikiwa
Komandi kuu ya vikosi vya ulinzi vya Syria imetangaza habari ya kufikiwa mapatano ya kusimamisha vita na kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano kote nchini Syria.
Komandi Kuu ya vikosi vya ulinzi vya Syria leo imetoa taarifa na kuashiria kuwa, kuanzia saa sita usiku wa tarehe 30 Disemba hatua zote za kijeshi zitasimamishwa nchini humo na kwamba makundi ya kigaidi ya Daesh na Jabhatul Nusra na yale yenye mfungamano na makundi hayo mawili hayajajumuishwa katika makubaliano hayo.
Komandi kuu ya vikosi vya ulinzi vya Syria imesisitiza kuwa makubaliano hayo yamefikiwa huko Syria ili kuunga mkono juhudi za kuutatrua kisiasa mgogoro wa nchi hiyo.
Kwa upande wake, Rais Vladimir Putin wa Russia ametangaza kuwa, tayari kumefikiwa makubaliano ya kusimamisha vita nchini Syria na kwamba pande husika zipo tayari kwa ajili ya kuanza mazungumzo ya kusaka amani nchini humo.
Rais wa Russia ameongeza kuwa, wawakilishi wa wapinzani wa Syria na serikali ya nchi hiyo wamekubaliana kusimamisha vita na kwamba Moscow itasaini nyaraka ya kusimamia makubaliano hayo ya Syria. Wapinzani na serikali ya Syria wamefikia muafaka wa kusimamisha mapigano nchini humo ikiwa zimepita siku kadhaa baada ya kukombolewa mji wa kistratejia wa Halab (Aleppo) baada ya kushikiliwa na magaidi kwa zaidi ya miaka minne na miezi mitano.