UN: Ubomoaji nyumba za Wapalestina unaofanywa na Israel umeongezeka mno
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mwaka huu unaomalizika wa 2016 umeshuhudia ongezeko la vitendo vya uvunjaji na ubomoaji nyumba za Wapalestina uliofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa, takwimu za kuvunjwa na kubomolewa na utawala wa Kizayuni wa Israel nyumba za Wapalestina huko Baytul Muqaddas Mashariki na katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan zinaonyesha kuwa, vitendo hivyo viliongezeka mno katika mwaka huu unaomalizika.
Sehemu moja ya ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa, hatua za Israel za kubomoa nyumba za Wapalestina zilishadidi mno mwaka huu na kwamba, hatua kama hizo hazijawahi kushuhudiwa huko Palestina katika kipindi cha miaka saba iliyopita.
Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa, kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu hadi tarehe 28 Disemba, utawala wa Kizayuni wa Israel umepelekea Wapalestina 1,593 kubaki bila makazi baada ya nyumba zao kuvunjwa huku hatua hiyo ikiathiri maisha ya Wapalestina 7,101.
Kuongezeka na kuendelea hatua za Israel za kubomoa majengo na nyumba za Wapalestina na ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala huo ghasibu ni kengele ya hatari kwa wanadiplomasia na makundi ya kutetea haki za binadamu.
Hivi karibuni Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 2334 linaloitaka Israel isitishe mara moja ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zilizoghusubiwa za Palestina.