Mashia na Masuni Iraq wajadili mustakbali baada ya kuangamizwa ISIS
Mirengo mikubwa zaidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na Suni katika Bunge la Iraq imeafikiana kuhusu namna ya kurejesha ustawi na amani katika nchi hiyo baada ya maangamizo tarajiwa ya kundi la kigaidi la ISIS au Daesh.
Viongozi wa Muungano wa Kitaifa wa Mashia Iraq (INA) na Muungano wa Masuni Iraq (IFC) wamefika mwafaka huo katika mkutano uliofanyika Jumatano katika nyumba ya Spika wa Bunge la Iraq, Salim al Jabouri ambaye ni kati ya viongozi wa IFC.
Katika mkutano huo, ambao ulifanyika baina ya Jabouri na Sayyed Ammar al Hakim kiongozi wa INA, pande mbili zilifikia mapatano ya kimsingi kuhusu namna Iraq itakavyoendeshwa baada ya kuangamizwa kundi la ISIS.
Kwa mujibu wa Jabouri, pande mbili zimeafikiana kuhusu umuhimu wa kuondoa ile nadharia ya 'mshindi anachukua kila kitu," huku wakisisitiza umuhimu wa kushirikiana ili kuijenga nchi hiyo ambayo tokea mwaka 2014 imekuwa ikikabiliana na ugaidi wa ISIS.
Siku ya Jumanne iliyopita Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al Abadi alisema itachukua miezi mitatu kuwatimua magaidi wa ISIS katika maeneo yote ya nchi hiyo.