Magaidi wa Daesh walipua daraja linalounganisha mji wa Mosul
Kamanda wa operesheni za kuukomboa mkoa wa Nainawa (Nineve) kaskazini mwa Iraq, amesema kuwa, genge la kigaidi na kitakfiri la Daesh, limeripua upande wa kulia wa daraja la Mto Tigris linalouonganisha mji wa Mosul na maeneo mengine.
Genge hilo la ukufurishaji limechukua hatua hiyo ili kuzuia jeshi la serikali linaloshirikiana na harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'ab kuingia mjini humo hasa baada ya jeshi hilo kupata mafanikio makubwa dhidi ya wanachama wa kundi hilo. Abdul-Amir Rashid Yarullah, Kamanda wa operesheni za kuukomboa mkoa wa Nainawa ameongeza kuwa, magaidi hao wanaopata himaya kutoka Marekani, Israel, Saudia na nchi nyingine za ndani na nje ya eneo, wametenda uharibifu huo wakati jeshi la serikali lilikuwa limeanza kudhibiti maeneo ya karibu na darala hilo muhimu.
Kabla ya hapo kamanda wa operesheni hizo za kuukomboa mkoa wa Nainawa alinukuliwa akisema kuwa, jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kudhibiti maeneo kadhaa yaliyokuwa yakikaliwa kwa mabavu na magaidi wa Daesh, ambapo kwa akali wanachama 277 wa genge hilo wameangamizwa. Kusonga mbele kwa jeshi la Iraq kumewafanya viongozi wa serikali kutangaza kuwa, siku za kuukomboa kikamilifu mji huo, zimekaribia.
Hatua ya kwanza ya kuukomboa mji wa Mosul ilikamilika tarehe 15 Disemba mwaka jana, ambapo jumla ya maeneo 40 yakiwemo maeneo mengine 56 ya upande wa mashariki mwa Mosul yalisafishwa kutoka mikononi mwa magaidi.