Saudia yaendeleza mashambulizi Yemen na kuua watu saba wa familia moja
Raia wa Yemen wasiopungua saba wameuawa katika mashambulizi ya hivi karibuni ya ndege za kivita za jeshi la Saudi Arabia nchini humo.
Televisheni ya al Aalam imeripoti kuwa, wanawake watatu na watoto wanne wa familia moja wameuawa katika mashambulizi yaliyofanywa na ndege za kivita za Saudi Arabia katika eneo la al Jah mkoani Jadida magharibi mwa Yemen. Ndege hizo vamizi za Saudia zimeushambulia pia mara kadhaa mji wa al Salif katika mkoa wa al Jadida magharibi mwa Yemen.
Habari zinasema kuwa kikosi cha makombora cha jeshi la Yemen na makundi ya kujitolea ya wananchi jana alasiri yalijibu mashambulizi na jinai za utawala wa Aal Saud kwa kuzishambulia ngome na vituo vya kijeshi vya jeshi la Saudi Arabia huko Najran kusini mwa nchi hiyo na kulisababishia hasara kubwa jeshi hilo. Katika mashambulizi hayo magari mawili ya jeshi la Saudi Arabia yameharibiwa huko Najran na Aisir baada ya kupigwa na makombora ya jeshi la Yemen. Raia wa Yemen zaidi ya elfu 11 wameuawa hadi sasa na mamilioni ya wengine wamekuwa wakimbizi tangu Saudi Arabia ikiungwa mkono na Marekani na Uingereza ianzishe uvamizi wake wa kijeshi huko Yemen mwezi Machi mwaka juzi.