Human Rights Watch yataka kusitishwa uuzaji silaha kwa Saudi Arabia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i23488-human_rights_watch_yataka_kusitishwa_uuzaji_silaha_kwa_saudi_arabia
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetoa ripoti likitaka kusimamishwa haraka iwezekanavyo uuzaji silaha kwa Saudi Arabia. Ripoti hiyo imebainisha kuwa utawala wa Saudia chini ya muungano wa kijeshi unaoungwa mkono na Marekani na Uingereza mwezi Machi mwaka juzi ulianzisha mashambulizi ya kijeshi huko Yemen na kuzishambulia kinyume cha sheria, nyumba, masoko, shule, viwanda na misikiti nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 14, 2017 23:07 UTC
  • Human Rights Watch yataka kusitishwa uuzaji silaha kwa Saudi Arabia

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetoa ripoti likitaka kusimamishwa haraka iwezekanavyo uuzaji silaha kwa Saudi Arabia. Ripoti hiyo imebainisha kuwa utawala wa Saudia chini ya muungano wa kijeshi unaoungwa mkono na Marekani na Uingereza mwezi Machi mwaka juzi ulianzisha mashambulizi ya kijeshi huko Yemen na kuzishambulia kinyume cha sheria, nyumba, masoko, shule, viwanda na misikiti nchini humo.

Ripoti hiyo ambayo imetegemea takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR imeongeza kuwa mashambulizi ya anga ya Saudi Arabia yameuwa na kujeruhi maelfu ya raia wa Yemen. Kuendelea na kuongezeka mashambulizi ya anga ya Saudi Arabia dhidi ya raia wa Yemen kumelipelekea shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch kulaani waziwazi jinai hizo za Saudia na kutaka kusimamishwa uuzaji wa silaha kwa nchi hiyo, licha ya serikali za Magharibi kulinyamazia kimya jambo ilo. Ni wazi kuwa utawala wa Aal Saud usingeweza kuendeleza mashambulizi ya anga mtawalia dhidi ya maeneo ya umma na makazi ya raia huko Yemen sambamba na kuuwa ovyo wanawake na watoto wa nchi hiyo, iwapo kusingekuwa na misaada ya aina mbalimbali za silaha na zana za kijeshi na pia uungaji mkono wa pande zote wa kilojistiki na kiintelijinsia wa nchi kama Marekani na Uingereza. Marekani katika miaka kadhaa ya hivi karibuni imeiuzia Saudia silaha za mabilioni ya dola. Aidha mwaka jana wa  2016 Marekani iliafiki kuiuzia Saudi Arabia anuai za silaha na makombora yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni moja na milioni mia moja ili kujaza tena maghala ya silaha za nchi hiyo ambazo zinatumika vitani huko Yemen. Si hayo tu, kwa mujibu wa takwimu rasmi za kampeni ya kupambana na biashara ya silaha, Saudi Arabia inatambulika kama mnunuzi mkubwa wa silaha za Uingereza; na kuanzia mwaka 2010 Riyadh ilinunua zana za kijeshi kutoka nchi hiyo zenye thamani ya pauni zaidi ya bilioni 6 na milioni 700. Mbali na ndege za kivita, Uingereza imeiuzia Saudia pia aina mbalimbali za makombora na mabomu; na uuzaji huo wa silaha kwa Saudia umeongezeka baada ya Riyadh kuanzisha vita huko Yemen.

Mauaji ya raia wa Yemen kwa kutumiwa silaha za Saudia inazonunua kutoka Marekani na Uingereza 

Ni dhahir shahir kwamba Marekani na Uingereza zimefumbia macho jinai na maafa yaliyosababishwa na muungano unaoongozwa na utawala wa Aal Saud katika uvamizi wa kijeshi wa miezi 22 huko Yemen ili kuendeleza shughuli za makampuni yao ya uundaji silaha, kujiongezea faida; na pia kuwapatia ajira  maelfu ya raia wa  nchi hizo katika makampuni hayo. Hatua hiyo  imeakisi kikamilifu muamala wa undumakuwili wa nchi za Magharibi zikiwemo Marekani na Uingereza kuhusu suala la kuheshimiwa na kulindwa haki za binadamu. Serikali za Marekani na Uingereza zimekuwa zikipuuza ripoti nyingi za mashirika ya kutetea haki za binadamu kuhusu mauaji ya raia wa Yemen na ubomoaji wa maeneo na taasisi za kiraia unaofanywa na ndege za kivita za Saudi Arabia na waitifaki wake, licha ya ripoti hizo kubainisha wazi jinai hizo; huku nchi hizo zikiendelea kuiuzia silaha na kuipatia misaada ya kijeshi Riyadh, ikiwemo misaada mbalimbali ya kiitelijinsia na zana za kivita. Si  mashirika ya kutetea haki za binadamu tu ndiyo yanayolalamikia na kulaani kuendelea kuuziwa Saudia aina mbalimbali za silaha yakiwemo mabomu ya vishada, bali hivi karibuni kamati ya bunge inayosimamia uuzaji silaha katika bunge la Uingereza pia iliitaka serikali ya nchi hiyo isimamishe kwa muda kuiuzia Saudia silaha kufuatia kushtadi mashinikizo ya fikra za waliowengi na ya jumuiya za kiraia zinazopinga vita. Katika fremu hiyo Chris White, mkuu wa kamati hiyo ambayo huko nyuma ilitaka pia kusimamishwa mauzo ya silaha kwa serikali ya Riyadh amekiri bayana kuwa kupuuzwa ripoti zinazoeleza kuwa utawala wa Saudia unatumia mabomu ya vishada na kuwauwa raia katika mashambulizi yake ya anga huko Yemen kumeitia dosari taswira ya Uingereza kimataifa. 

Mabomu ya vishada yanayotumiwa na jeshi la Saudi Arabia kuwaua raia wa Yemen