Marekani yaendelea kusaidia magenge ya kigaidi nchini Syria
Huku juhudi za kuitisha mazungumzo ya amani ya Syria huko Astana mji mkuu wa Kazakhstan zikiendelea, vyombo vya habari vimetangaza kuwa, Marekani imeongeza misaada yake kwa magenge ya kigaidi yanayofanya mauaji dhidi ya raia na maafisa wa serikali ya Rais Bashar al Assad wa nchi hiyo.
Shirika la habari la Fars limelinukuu gazeti la USA Today likiripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, misaada mipya ya kijeshi ya Marekani kwa magenge yenye silaha dhidi ya Rais Bashar al Assad huko Raqqah, itatumwa tena karibuni hivi.
Silaha hizo mpya za Marekani zinatumwa kwa magenge ya kigaidi nchini Syria kwa njia ya anga. John Dorrian, msemaji wa muungano wa Marekani unaodaiwa kupambana na genge la kitakfiri la Daesh amesema, silaha hizo ni muhimu kwa ajili ya vita vya chini kwa chini.
Mwezi Disemba mwaka jana, Rais Barack Obama wa Marekani aliondoa baadhi ya vizuizi vya kutumwa misaada ya kijeshi ya Marekani kwa makundi ya kigaidi nchini Syria.
Hivi karibuni kiongozi mmoja wa genge la kigaidi la Jabhatun Nusra lililojibadilisha jina na kujiita Fat'h al Sham nchini Syria alifichua kuwa, wanapata misaada mingi ya silaha kutoka kwa Marekani.
Wakati huo huo vyombo vya habari vimeripoti kuwa, baada ya kushindwa magaidi huko Halab (Aleppo), maafisa wa serikali ya Syria waligundua shehena kubwa ya silaha za Marekani zilizotumwa kwa magenge ya kigaidi likiwemo la Jabhatun Nusra.
Hivi karibuni pia, John Kerry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alikiri kuwa, nchi yake haikuzuia kuanzishwa genge la ISIS kwa ajili ya kuipindua serikali ya Rais Bashar al Assad, bali hata iliwapa silaha magaidi wa kundi hilo kukabiliana na serikali ya Syria.