Kuongezeka wimbi la umasiki nchini Saudia
Philip Alston, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya ongezeko la umasikini na masuala ya haki za wanawake duniani amesema kuwa, kinyume na inavyodhaniwa, nchini Saudia kuna maeneo mengi ambayo wakazi wake ni masikini wa sana.
Alston amesema kuwa bima ya jamii nchini Saudia ni mseto wa mipango isiyofaa, isiyokuwa ya muda mrefu, isiyo na uwiano, na mbaya zadi haiwezi kukidhi mahitaji ya watu wasikini kwenye jamii. Kwa ajili hiyo ripota huyo ameitaka serikali ya Riyadh kutambua rasmi bima ya jamii kama haki kwa ajili ya raia wa nchi hiyo. Naye Sara Elhaf mwandishi wa habari wa kanali ya Al-Mayadin, ameripoti kwamba, nchini Saudia nje ya majengo ya kasri na ya kifahari, kuna ukiukaji wa kupindukia wa uhuru na haki za kiraia hususan haki za wanawake kutokana na mfumo mbaya wa kiutawala nchini humo.
Ameongeza kuwa, Aal Saud wameharibu uchumi wa kitaifa kwa kuufanya utegemezi tu mafuta. Inafaa kufahamu kwamba, nchini humo kuna wanawafalme elfu tisa ambao kwa mwezi wanapata kiasi cha riale milioni tatu hadi milioni 120 fedha za Saudia kila mmoja katika hali ambayo raia wa kawaida wamesalia katika umasikini mkubwa. Katika miaka ya hivi karibuni hususan baada ya njama za kushusha bei ya mafuta katika soko la dunia kulikofanywa na watawala wa nchi hiyo kwa ushirikiano wa madola ya Magharibi, kumeshuhudiwa hali mbaya ya maisha na hivyo kuwafanya wananchi wa taifa hilo kuanzisha wimbi la malalamiko dhidi ya utawala huo. Katika mazingira hayo viongozi wa Saudia sanjari na kutoa mapendekezo yaliyo nje ya uwezo wao, wanakusudia kuwashughulisha raia wa nchi hiyo na masuala ya pembeni ili kupunguza wimbi la malalamiko yao. Katika miezi ya hivi karibuni Saudia imeathirika pakubwa na utekelezaji wa siasa zake za hiana katika eneo la Mashariki ya Kati likiwemo suala zima la kushusha kwa makusudi bei ya mafuta. Katika kipindi hiki Riyadh imejikuta akiathirika pakubwa na siasa hizo mbovu. Wakati huo huo takwimu zinaelezea ongezeko la mfumuko wa bei za bidhaa wa zaidi ya asilimia 10 kiasi ambacho ni cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 30 iliyopita.
Kiasi hicho kimeendana na ongezeko la ukosefu wa ajira na pia kuporomoka pakubwa kwa hisa za nchi hiyo kwa asilimia 10. Bei ya vyakula na makazi nchini humo imeongezeka mara dufu. Licha ya Saudia kujiingizia kiasi cha mabilioni ya dola kinachotokana na pato la mafuta kwa mwaka, lakini karibu asilimia 70 ya raia wake hawaridhii hali mbaya ya uchumi wa nchi hiyo. Hii ni kwa kuwa Riyadh imejikita tu katika ununuzi wa silaha za kijeshi huku ikifumbia macho malalamiko ya wananchi, ununuzi ambao unafanyika huku nchi hiyo ikiwa haikabiliwi na tishio lolote. Aidha ufisadi wa kifedha na ki-idara wa wanawafalme wa nchi hiyo na kadhalika matukio ya miaka ya hivi karibuni katika nchi za eneo kama vile Syria, Iraq na Yemen, umeharibu zaidi uchumi wa taifa hilo. Kuendelea siasa za watawala hao dhidi ya raia katika uwanja wa kisiasa, kijamii, kisheria na kiuchumi kumekuwa na taathira mbaya katika nyuga tofauti za maisha ya raia hao. Kwa utaratibu huo tunaweza kusema kuwa, suala la uchumi wa Saudia kufikia nukta ya mgogoro, ni ishara ya kuporomoka uchumi na kuongezeka umasikini ndani ya taifa hilo la Kiarabu.