Israel yadharau azimio la UN; yaidhinisha ujenzi wa nyumba mpya 566
Mamlaka za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel zimeidhinisha vibali vya ujenzi wa nyumba mpya 566 za walowezi wa Kizayuni katika mji wa Baitul Muqaddas Mashariki unaoukalia kwa mabavu.
Uidhinishaji huo uliotangazwa leo umefanyika siku mbili baada ya kuapishwa Donald Trump kuwa rais mpya wa Marekani, huku maafisa wa utawala wa Kizayuni wakieleza kwamba hatua hiyo ilikuwa imesitishwa kusubiri kumalizika kipindi cha utawala wa Barack Obama ambaye serikali yake imekuwa ikikosoa ujenzi wa vitongoji.
Meir Turjeman, Naibu Meya wa Baitul Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu amesema: "Kanuni za mchezo zimebadilika baada ya Donald Trump kuwa rais. Mikono yetu sasa haifungiki tena kama ilivyokuwa wakati wa Barack Obama. Hatimaye sasa tunaweza kujenga".
Kwa mujibu wa Turjeman, maafisa wa utawala haramu wa Israel katika mji wa Baitul Muqaddas wamepitisha mipango ya ujenzi wa nyumba hizo ambao ulikuwa umeakhirishwa kwa ombi la Waziri Mkuu wa utawala huo ghasibu Benjamin Netanyahu katika kipindi cha mwezi uliopita wa Desemba wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipopitisha azimio la kuitaka Israel isitishe ujenzi wa vitongoji katika aradhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.
Naibu Meya wa Quds tukufu inayokaliwa kwa mabavu ameeleza pia kwamba mipango ya utoaji vibali vipya vya ujenzi wa nyumba nyingine 11,000 katika mji huo iko mbioni.
Ujenzi wa vitongoji katika eneo la Ufukwe wa Magharibi linalokaliwa kwa mabavu ni hatua haramu kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Hii ni katika hali ambayo baina ya mwaka 2009 na 2014 Israel imepanua kwa asilimia 23 ujenzi wa vitongoji katika eneo la Ufukwe wa Magharibi ikiwemo Baitul Muqaddas Mashariki.
Wakati huohuo Nabil Abu Radeneh, msemaji wa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amelaani mipango mipya ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kuutaka Umoja wa Mataifa uchukue hatua hususan kwa kuzingatia azimio la karibuni la Baraza la Usalama la umoja huo.
"Umefika wakati wa kuacha kuamiliana na Israel kama dola lililo juu ya sheria", amesema msemaji huyo wa Mahmoud Abbas…/