Wakimbizi wa Kiiraqi warejea katika maeneo yaliyokombolewa huko Mosul
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i24251-wakimbizi_wa_kiiraqi_warejea_katika_maeneo_yaliyokombolewa_huko_mosul
Maafisa wa Iraq wameeleza kuwa maelfu ya wakimbizi wamerejea makwao katika maeneo yaliyokombolewa hivi karibuni huko Mosul makao makuu ya mkoa wa kaskazini wa Nainawa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 26, 2017 00:11 UTC
  • Wakimbizi wa Kiiraqi warejea katika maeneo yaliyokombolewa huko Mosul

Maafisa wa Iraq wameeleza kuwa maelfu ya wakimbizi wamerejea makwao katika maeneo yaliyokombolewa hivi karibuni huko Mosul makao makuu ya mkoa wa kaskazini wa Nainawa.

Maafisa hao wamesema kuwa wakimbizi hao raia wa Iraq wameondoka katika kambi walizokuwa wakiishi na kurejea katika makazi yao baada ya kukombolewa eneo la mashariki mwa Mosul. Hilo ni wimbi kubwa zaidi la wakimbizi waliorejea katika makazi yao tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka jana hadi sasa. Umoja wa Mataifa pia umetangaza kuwa Wairaqi wasiopungua elfu 22 kati ya 180,000  ambao walilazimika kuwa wakimbizi kutokana na mapigano huko Mosul na katika maeneo ya karibu na mji huo, tayari wamerejea makwao. Viongozi wa serikali ya Baghdad wamesema kuwa oparesheni ya kuwarejesha wakimbizi katika maeneo yaliyokombolewa huko Mosul ilitekelezwa mara mbili kwa wiki katika kambi za al Khazar na Hassan al Sham.

Wakimbizi wa Iraq wakiwa kambini kabla ya kurejea makwao Mosul 

Oparesheni ya kuukomboa mji wa Mosul makao makuu ya mkoa wa Nainawa kwa kuanza na maeneo sita ya mji huo, ilianza Oktoba 17 mwaka jana kwa agizo la Haidar al Abadi Waziri Mkuu wa Iraq ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote ya nchi hiyo. Hivi sasa eneo la mashariki mwa Mosul limekombolewa kikamilifu kutoka mikononi mwa magaidi wa kundi la Daesh.