Wakimbizi wa Afrika huko Israel walalamikia unyanyasaji
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i24323-wakimbizi_wa_afrika_huko_israel_walalamikia_unyanyasaji
Mamia ya wakimbizi wa Kiafrika wamefanya maandamano nje ya Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset), kukosoa sera za kikatili na kibaguzi za Tel Aviv dhidi yao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 27, 2017 10:21 UTC
  • Wakimbizi wa Afrika huko Israel walalamikia unyanyasaji

Mamia ya wakimbizi wa Kiafrika wamefanya maandamano nje ya Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset), kukosoa sera za kikatili na kibaguzi za Tel Aviv dhidi yao.

Mamia ya waandamanaji hao walimiminika nje ya Bunge na Mahakama ya Juu ya utawala huo wa Kizayuni jana Alkhamisi, kushiriki maandamano ya kulalamikia sera za utawala huo bandia zinazotaka wakimbizi hao wakamatwe kwa umati na kutimuliwa.

Baadhi ya wakimbizi hao wa Kiafrika walikuwa wamebeba mabango yenye ujumbe unaosema "Maisha ya Weusi ni ya Thamani" huku baadhi ya mabango yakiwa na maandishi yanayosema, "Msitulazimishe Tuondoke Tukatafute Hifadhi Kwingine".

Uzio wa kibaguzi katika mpaka wa Misri na Israel

Aidha waandamanaji hao wa Kiafrika aghalabu yao kutoka nchi za Sudan na Eritrea walikuwa wamebeba picha za baadhi ya wakimbizi wenzao ambao wametimuliwa na utawala huo wa Kizayuni na wengine wanaozuiliwa kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa waandamanaji hao wa Kiafrika, zaidi ya raia elfu 10 hususan kutoka Sudan na Eritrea wanazuiliwa chini ya mazingira magumu katika gereza la Holot eneo la Negev, huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel. Waafrika wanaotafuta hifadhi huko Israel ni zaidi ya 45,000.

Mwaka 2015, gazeti la Washington Post liliripoti kuwa, utawala haramu wa Israel umetumia zaidi ya dola milioni 350, kujenga uzio katika mpaka na Misri, ili kuzuia wakimbizi wa Kiafrika kuingia katika ardhi walizozighusubu za Wapalestina.