Saudi Arabia yazuia msaada wa chakula kufikishiwa wananchi wa Yemen
Utawala wa Saudi Arabia umezuia kufikishiwa misaada ya chakula kwa wananchi wa Yemen baada ya kuizuia katika bandari ya al-Hadida meli iliyokuwa imebeba shehena ya chakula kwa ajili ya wananchi wa nchi hiyo.
Kanali ya Televisheni ya al-Alam imetangaza kuwa, Saudia imeizuia kutia nanga katika bandari ya al-Hadida meli iliyokuwa imebeba shehena ya ngano. Inaelezwa kuwa, Saudia iliitaka meli hiyo isitie nanga katika bandari ya al-Hadida na badala yake ikatie nanga katika bandari ya Jeddah nchini Saudia.
Cha kushangaza zaidi ni kwamba, meli hiyo ya mizigo ilikuwa na kibali cha muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia yenyewe ambao umekuwa ukiendesha operesheni za kijeshi dhidi ya Yemen.
Hatua hiyo imelalamikiwa vikali na mashirika mbalimbali ya utoaji misaada ya kibinadamu ambayo yameitaja kuwa si ya kibinadamu. Bandari ya al-Hadida ndio njia pekee ya kufikia miji ambayo iko chini ya udhibiti wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen.
Saudia, kwa kushirikiana na waitifaki wake, ilianzisha hujuma za kila upande dhidi ya Yemen tarehe 26 Machi mwaka 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani kibaraka wake Abdrabbuh Mansur Hadi, rais wa zamani wa Yemen ambaye alijiuzulu nafasi hiyo na kukimbilia Saudia.
Hata hivyo licha ya Riyadh kufanya mauaji na uharibifu mkubwa nchini Yemen, imeshindwa kufikia malengo yake nchini humo.