Jeshi la Iraq: Magaidi wa ISIS wamezingirwa kikamilifu mjini Mosul
Msemaji wa Harakati ya Kujitolea ya Wananchi nchini Iraq amesema kuwa, wanachama wa genge la kigaidi na ukufurishaji wa Daesh (ISIS) wamezingirwa kikamilifu katika eneo la magharibi mwa mji wa Mosul nchini humo.
Ahmad al-Assad sanjari na kuelezea kukamilika operesheni za wapambanaji wa harakati hiyo ya wananchi katika maeneo ya magharibi mwa mji wa Mosul kuelekea mpaka wa Syria, amesema kuwa, wapiganaji wa genge hilo la kigaidi hawana uwezo wa kutoka eneo hilo wala kwenda upande wa pili yaani Syria.
Al-Assad ameongeza kuwa, wanachama wa kundi hilo wamekwama na kuzingirwa katika eneo lililo kati ya mji wa Tal-Afar na pwani ya magharibi mwa mji wa Mosul na kwamba operesheni hiyo ni utangulizi wa operesheni kabambe ambayo itaanza hivi karibuni kwa ajili ya kuyakomboa maeneo yaliyosalia ya mji wa Sinjar nchini humo. Hii ni katika hali ambayo vyombo mbalimbali nchini Iraq vimetangaza habari ya kuangamizwa mmoja wa vinara wa ngazi za juu wa kundi la Daesh kwa jina la Abu Suhaid katika mji ulio kilometa 63 kaskazini mwa mji wa Baqubah na kwamba gaidi huyo ameuawa kwa shambulizi la anga la jeshi la Iraq.
Wakati huo huo maafisa wa Iraq wameeleza kuwa jumla ya watu elfu 49 waliokuwa wameyakimbia makazi yao mjini Mosul, tayari wamerejea makwao katika maeneo yaliyokombolewa hivi karibuni katika mji huo ambao ni makao makuu ya mkoa wa kaskazini wa Nainawa.